Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mradi wa Matanki ya Mafuta Kuifanya Tanzania Kitovu cha Biashara Kikanda
Mar 03, 2026
Mradi wa Matanki ya Mafuta Kuifanya Tanzania Kitovu cha Biashara Kikanda
Rais wa Tanzania wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Matanki 15 ya kupokea na kusambaza Mafuta, katika Viwanja vya Madani, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Na Rajabu Sodangu – MAELEZO

Rais wa Tanzania wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema mradi wa ujenzi wa matanki ya mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam utakuwa chachu ya kuimarisha uchumi wa taifa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na maendeleo kwa nchi jirani.

Rais Samia ametoa kauli hiyo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matanki 15 ya kupokea na kusambaza mafuta, iliyofanyika leo Machi 3, 2026 katika viwanja vya Madani, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza ujenzi wa matanki hayo yenye ujazo wa mita za ujazo 374,000, kwa gharama ya Shilingi bilioni 664.6 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24, ifikapo Februari 2027 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 41 ya utekelezaji.

Rais Samia amesema uwekezaji huo wa Serikali ni hatua ya kimkakati katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara na uwekezaji wa kikanda na kimataifa. “Uwekezaji wa Serikali katika ujenzi wa matanki ya kupokea mafuta ni hatua ya kimkakati katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji wa kibiashara wa kikanda na kimataifa,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa meli kusubiri kuhudumiwa bandarini, kupunguza msongamano, kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na hatimaye kuongeza mapato ya taifa kupitia ushuru wa forodha.

Sambamba na hilo, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Usimamizi w Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, kwa ubora unaozingatia viwango vya kimataifa na kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa mradi huo utaimarisha usalama wa uhifadhi wa mafuta nchini.

Aidha, ameitaka Wizara ya Nishati kujiimarisha kimkakati katika uhifadhi wa mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kimataifa, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi