Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajia kuwa na wapiga kura 34,746, 638 wanaotarajiwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura baada ya uboreshaji wa daftari hilo katika uchaguzi mkuu wa unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Tume hiyo imesema idadi hiyo imekuja kwa kuzingatia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambapo wapiga kura wapya 5,586,433 wanatarajiwa kujiandikisha sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29, 754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/2020.
Hayo yamebainishwa leo Machi 05,2025 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi toka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi-INEC Bw. Ramadhan Kailima, wakati akitoa mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, kwa wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na Wadau.
Bw. Kailima amesema, kufuatia takwimu za sensa hiyo ya watu na makazi ya mwaka 2022, wapiga kura 4,369,531 inatarajiwa wataboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494, inatarajiwa wataondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye daftari hilo.
Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kailima amesema,Tume hiyo inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura waliopo 3,427,917 ambapo baada ya uandikishaji, mkoa huo utakuwa na wapiga kura 4,071,337
Aidha, imesema idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana kuwepo kwa Watanzania wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/2020, lakini kwa sababu moja au nyingine, hawakuweza kujiandikisha.
Pia amesema, tume hiyo imeshakamilisha idadi ya idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura, ambapo imeridhia kufanyika kwa mabadiliko ya idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka vituo 40,126, hadi kufikia vituo 40,170 kwa kurejesha vituo 44 vya kata 11 za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.