Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 77 katika Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya afya.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera jijini Mbeya, wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na mkuu wa mkoa huyo, pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri, Mkutano huo unaratibiwa na Idara ya Habari (Maelezo), ukiwa na lengo la kuhabarisha umma juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika mikoa na Halmashauri zake kupitia programu ya Tumewasikia Tumewafikia.
“Kuanzia mwaka 2021/22 hadi kuishia Desemba, 2023, Mkoa umepokea jumla ya shilingi bilioni 77.67 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Sekta ya Afya baadhi ikiwemo ujenzi na ununuzi wa vifaa tiba katika Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda (Meta) Mbeya kwa shilingi bilioni 17.75,” ameeleza Mhe. Homera
Aidha, amebainisha kuwa fedha hizo zimetekeleza mradi wa ujenzi wa Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa gharama ya shilingi bilioni 5.37 na ujenzi wa Vituo vya Afya nane vya Kata katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kupitia Fedha za Tozo za Miamala ya Simu, Vituo hivyo ni Kifunda, Kambikatoto, Itunge, Njisi, Mahongole, Itagano, Swaya na Ndanto kwa gharama ya shilingi bilioni nne.
Vilevile, Mhe. Homera amesema kuwa, fedha hizo zimepanua miundombinu katika hospitali zote za Wilaya ndani ya Mkoa wa Mbeya ikiwemo ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje, majengo ya dharura, wodi za wanaume na wanawake, pamoja na miundombinu mingine na shilingi bilioni 3.04 zimetumika katika ujenzi wa zahanati 11 na vituo vya afya tatu.
“Jumla ya Shilingi billioni 4.2 zilipokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya sekta ya Afya, miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa OPD, RCH na jengo la wagonjwa katika hospitali za Wilaya za Chunya (milioni 800), kuendeleza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe (bilioni 1) pamoja na kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela kwa Shilingi bilioni 900 na jumla ya Shilingi bilioni 3.1 zilipokelewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Mkoa wa Mbeya,” amefafanua Mhe. Homera.
Mbali na hayo, Mhe. Homera ameeleza kuwa, jumla ya shilingi bilioni 1.405 zilipokelewa kwa ajili ya kutekeleza programu ya usafi wa mazingira katika Halmashauri sita za Mbeya, Busokelo, Kyela, Rungwe, Mbarali na Chunya.