Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za mfungo mwema kwa waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu kote nchini, walionza mfungo wa Kwaresma na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Katika salamu alizozitoa kupitia mitandao yake ya kijamii, Rais Samia amesema ni wakati wa Watanzania kuliombea Taifa amani, umoja, mshikamano na ustawi kwa wote akimuomba Mwenyezi Mungu azipokee funga, sala na sadaka za Watanzania.

“Ninawatakia Wakristo wote Kwaresma njema na yenye baraka mnapoanza safari hii takatifu kwa ibada ya Jumatano ya Majivu. Kipindi hiki muhimu kiimani kiwe fursa ya kutafakari kwa kina, kuimarisha uhusiano wenu na Mwenyezi Mungu, na kudumu katika sala, funga na matendo ya huruma” amesema Rais Samia
Kwa upande wa upande wa Waumini wa dini ya Kiislamu Rais Samia amewatakia mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani akitoa wito kwa waumini hao kuiombea Tanzania amani, umoja, mshikamano na ustawi kwa wote.

“ Nawatakia Waislamu wote kheri na mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Tusujudu kwa shukrani mbele za Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujalia neema adhimu ya kuufikia tena mwezi huu katika imani. Tunapotekeleza nguzo hii muhimu, tumwombe atujalie kudumu katika ibada na upendo kwake na jamii na akaipokee funga yetu. Katika kufunga na kusujudu mbele zake sote tuendelee kuiombea nchi yetu amani, umoja, mshikamano na ustawi kwa wote” amesema Rais Samia.