Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka wananchi kuheshimu matumizi bora ya ardhi na kuonya kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya kiburi vinavyochochea migogoro katika jamii.
Akizungumza Februari 18, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ndungu, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Waziri Mkuu amesema ukiukwaji wa matumizi sahihi ya ardhi unachangia kuondoa upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi.

“Kila mmoja aheshimu matumizi bora ya ardhi, sasa imezuka tabia ya kiburi, mtu anaona shamba la mtu anakwenda anasimama analisha mifugo yake mazao ya mkulima kama analisha majani, hili halikubaliki na wote wanaofanya kiburi tutashughulika nao maana wanatupeleka katika uvunjifu wa amani na kuondoa upendo miongoni mwetu,” amesema Dkt. Nchemba.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia sheria na taratibu za matumizi ya ardhi ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima, huku akiwahimiza viongozi wa maeneo kuhakikisha wanatatua changamoto hizo kwa haki na kwa kuzingatia sheria.
“Nawaomba msibaguane, kwenye nchi yetu wakulima na wafugaji wanaishi pamoja na katika maeneo mengine wanaofunga ndio wanaolima” amehimiza Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa matumizi sahihi ya ardhi ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na akatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kulinda rasilimali hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.