Tatizo la maji katika Mji wa Ludewa linatarajiwa kuwa historia baada ya Serikali kutenga shilingi bilioni 7.4 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaomaliza kabisa changamoto hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mheshimiwa Olivanus Thomas, wakati akizungumza katika kijiji cha Muhoro kwenye hafla ya kupokea na kushuhudia uwasilishaji wa mabomba ya mradi huo.

Mhe. Olivanus amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha fedha hizo, akieleza kuwa hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa wananchi wa Ludewa ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Ameeleza kuwa maandalizi ya chanzo cha maji katika eneo la Ilunga (intake) yamekamilika, huku matenki makubwa tayari yakijengwa katika maeneo ya Mdambanyafu, Kilimahewa na Mdonga kwa ajili ya kuhifadhi na kusambaza maji. Changamoto iliyokuwa imebaki ni kuunganisha maji kutoka chanzo hadi kwenye matenki hayo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema mabomba makubwa ya nchi 10 yameshawasili na yatawekwa kusafirisha maji kwa umbali wa kilometa 21.5 kutoka Ilunga hadi kwenye matenki akibainisha kuwa hatua inayofuata ni ujenzi wa mfumo wa uchujaji ili kuhakikisha maji yanayowafikia wananchi yanakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratias, amesema upatikanaji wa maji ya uhakika utaimarisha mazingira ya uwekezaji na kusaidia kupokea miradi mikubwa inayotarajiwa wilayani humo. Hata hivyo, aliwataka wananchi kulinda vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa sheria ndogo za Halmashauri pamoja na Sheria ya Mazingira zitasimamiwa kikamilifu dhidi ya waharibifu.
Mradi huo unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji mjini Ludewa na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo lenye takribani watumiaji wa maji 13,000.