Serikali imepanga kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 460 zinazotarajiwa kutumika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuweza kuufungua kibiashara na kuchochea fursa nyingi za kimaendeleo katika mkoa wa Kigoma.
Aidha, Bilioni 21 zimetolewa kwa ajili ya miradi mingine ya nyongeza ambayo itagusa jamii inayozunguka katika miradi ikiwemo ujenzi wa Shule, Soko, Miundombinu ya Maji Safi na Taka na Vituo cha Mabasi katika Wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyovu mara baada ya kukagua hatua ya ujenzi wa barabara ya Kanyani – Kidyama – Mvugwe (km 70.5), Njia panda ya Kasulu – Manyovu (km 68.25) pamoja na eneo patakapojengwa Kituo cha Kisasa cha Pamoja cha Manyovu/Mugina (OSBP) mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Naibu Waziri huyo amezitaja barabara ambazo zinatekelezwa kwa fedha hizo ikiwa ni ujenzi wa barabara ya Njia panda ya Nduta – Kabingo (km 62.5), Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini (km 25.9), Mvugwe – Njiapanda ya Nduta (km 59.35), Kanyani – Kidyama – Mvugwe (km 70.5), Njia panda ya Kasulu – Manyovu (km 68.25) ambazo zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2023.
“Serikali imeamua kuweka wakandarasi wengi katika mkoa huu kwa kuwa Kigoma haukuwa umefunguka kwa barabara za lami sasa zimeanza kujengwa hivyo tunawajibu kama wananchi kulinda miundombinu hii na kujiweka tayari kwa kufanya biashara na mikoa mingine ya jirani ili kujiongezea kipato”, amefafanua Kasekenya.
Ameongeza kuwa tayari wakandarasi wapo eneo la kazi kutokea Kigoma ukielekea Tabora kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Malagarasi (km 51.1) na Kazilambwa – Chagu (km 36) kwa kiwango cha lami.
Katika kufungua Mkoa wa Kigoma na Katavi, Mhandisi Kasekenya amesema kuwa tayari mkandarasi amekwishaanza ujenzi kutokea Mpanda (km 50) kuelekea Uvinza ili kupunguza umbali wa safari ukitokea Katavi.
“Tuna barabara tatu kubwa ambazo zinaunganisha Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine ambazo ni barabara ya Kibondo, Tabora, na Mpanda na tayari wakandarasi wameshaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami”, ameeleza Naibu Waziri Kasekenya.
Aidha, Wakala wa Barabara (TANROADS), umeshaanza usanifu wa kina wa barabara ya Kalela – Munzeze – Kirungu – Janda – Bukuba - Buhigwe (km 57.35), Buhigwe – Nyamugali - Muyama – Katundu (km 120) kwa ajili ya maandalizi ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma, amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwasimamia wakandarasi wote waliopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo ili kuhakikisha Mkoa wa Kigoma unafunguka na kurahasisha shughuli za usafirishaji na mikoa jirani pamoja na nchi jirani.
“Nikuhakikishie Naibu Waziri TANROADS tuko bega kwa bega kusimamia miradi hii licha ya changamoto za mvua na zinginezo watakamilisha kwa wakati na ubora uliosanifiwa”, amesema Mhandisi Choma.
Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Kigoma katika ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea mkoani humo.