Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zaidi ya Bilioni 300 Zatekeleza Miradi ya Maendeleo Songwe
Jan 30, 2024
Zaidi ya Bilioni 300 Zatekeleza Miradi ya Maendeleo Songwe
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis Michael akizungumza leo Januari 30, 2024 jijini Mbeya, wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na mkuu wa mkoa huyo pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri. Mkutano huo unaratibiwa na Idara ya Habari (Maelezo) ukiwa na lengo la kuhabarisha umma juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika mikoa na wilaya hapa nchini kupitia programu ya Tumewasikia Tumewafikia.
Na Lilian Lundo - Maelezo

Serikali ya Awamu ya Sita tangu imeingia madarakani imetoa jumla ya shilingi bilioni 343.43/-kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Songwe.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis Michael Januari 30, 2024 jijini Mbeya, wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na mkuu wa mkoa huyo, pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri. Mkutano huo unaratibiwa na Idara ya Habari (Maelezo), ukiwa na lengo la kuhabarisha umma juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika mikoa na wilaya hapa nchini kupitia programu ya Tumewasikia Tumewafikia.

Mhe. Michael amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, Mkoa wa Songwe umepokea jumla ya shilingi bilioni 343.43 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, katika sekta ya Elimu, Afya, Maji, Nishati, Miundombinu, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uwezeshaji Wananchi pamoja na Mazingira.
 
“Kabla ya mwaka 2021 mkoa ulikuwa na jumla ya shule za Awali na Msingi 452 hadi Desemba 2023, mkoa una shule 519, ikiwa na ongezeko la shule 67. Mwaka 2021 idadi ya wanafunzi walikuwa 270,784 hadi desemba 2023 mkoa una jumla ya wanafunzi 286,189, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 15,405. Idadi ya walimu waliokuwepo kabla ya mwaka 2021 ni 3,874 kufikia Desemba 2023 mkoa una walimu 4,074, ambao ni ongezeko la walimu 200,” amesema Mhe. Michael.

Ameendelea kusema kuwa, kuanzia Mwezi Machi 2021 hadi Disemba 2023, mkoa huo  umepokea jumla ya  shilingi bilioni 23.76 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu wa shule za Awali na Msingi, ambapo kati ya fedha hizo  shilingi bilioni 13.95 zilitolewa kwa ajili  ya ujenzi wa miundombinu ya shule za Awali na Msingi na shilingi bilioni 9.80 kwa ajili ya uendeshaji wa Shule za Msingi (Elimu Bila Malipo).
 
Kwa upande wa Elimu Sekondari, kabla ya mwaka 2021 mkoa ulikuwa na jumla ya shule za Sekondari 120 hadi Disemba 2023 mkoa una shule 153, ikiwa ni ongezeko la  shule  33. Idadi ya wanafunzi kabla ya mwaka 2021 walikuwa 52,097 hadi Disemba 2023 mkoa una jumla ya wanafunzi 57,424, ikiwa ni ongezeko la  wanafunzi 5,327. Aidha idadi ya walimu wa Sekondari waliokuwepo kabla ya mwaka 2021 ni 1,836, na kufikia Disemba 2023 mkoa una walimu 3,874, ikiwa ni ongezeko la walimu 2,038.

“Kuanzia Mwezi Machi 2021 hadi Desemba 2023, mkoa umepokea jumla ya shilingi 55.07 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za sekondari na ruzuku ya uendeshaji wa shule, ambapo  kati ya  fedha hizi shilingi bilioni 10.49 ni kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji wa shule za sekondari na shilingi bilioni 25.81 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za sekondari,” amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa.
 
Kwa upande wa Sekta ya Afya, kabla ya mwaka 2021, Mkoa ulikuwa na jumla ya vituo 205 vya kutolea huduma za afya ambapo vimeongezeka hadi vituo 263 kufikia Disemba 2023. Kati ya vituo hivyo hospitali ni 10 ambazo ni sawa na 3.8%, vituo vya afya 23 sawa na 8.7% na zahanati 230 sawa na asilimia 87.5%. Aidha, miongoni mwa vituo hivyo vituo vya Serikali ni 214 sawa na asilimia 81.4% na vituo vya binafsi pamoja na vituo vya mashirika ya dini ni 49 sawa na asilimia 18.6.
 
“Katika kipindi cha 2021/2022 hadi Disemba 2023, Mkoa umepokea jumla ya shilingi 38.83 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Sekta ya Afya katika halmashauri zake,” amesema Mhe. Michael.

Aidha, mkoa huo umepokea jumla ya shilingi bilioni 39.77 kwa ajili ya utengenezaji na ukarabati wa barabara za TANROADS. Pia umepokea shilingi bilioni 42.07 kwa ajili ya utengenezaji na ukarabati wa barabara za TARURA.

 Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema kuwa, jumla ya shilingi 38.63 zilipokelewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na ukarabati katika sekta ya maji, ambapo hali ya upatikanaji wa maji safi kwa mwaka 2020/2021 ilikuwa ni 54.3% vijijini na 44.5% mijini. Katika kipindi cha awamu ya sita hali ya upatikanaji wa maji safi na salama imeongezeka kufikia 78.8% vijijini na 50.6% mijini.
 
Vile vile, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mkoa huo umepokea jumla ya shilingi bilioni 103.32/- kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya kilimo, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 75.14/- ni thamani ya ruzuku ya mbolea kwa wakulima 109,373 ambapo jumla ya tani 111,276.345 za mbolea zimetumika kwenye mashamba ya wakulima katika kipindi cha Awamu ya Sita.
 
“Tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasikiliza wananchi na kuendelea kutatua changamoto zao,” amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi