[caption id="attachment_46385" align="aligncenter" width="750"] : Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akisisitiza jambo wakati akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo tarehe 31 Agosti 2019 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali.[/caption]
Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema kuwa zabuni ya ununuzi wa treni 5 za umeme zilizokamilika za abiria utawezesha kuanza kwa huduma ya usafirishaji kati ya Jiji la Dar es Salaam na Morogoro na baadae Dodoma.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Serikali hadi kufikia Agosti 2019.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali imeanza zabuni hiyo ambayo itawezesha kununuliwa kwa vichwa 22 vya Treni (vitano vya mafuta yaani Diesel Locomotive na 17 vya umeme yaani Electrical Locomotive), pamoja na mabehewa ya abiria 60 na 1430 ya mizigo.
“Treni tano (5) zilizokamilika (Electrical Multiple Unit) za abiria zenye mabehewa nane (8) kila moja na vichwa viwili kwa ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na kisha Dodoma zitawezesha watanzania kuanza kutumia usafiri wa kisasa na wa gharama nafuu hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi.” Alisisitiza Dkt. Abbasi
Akifanua amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ikiwemo ya reli ndio maana imeweka mkazo katika ujenzi wa mradi huo wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR)
Kuanza kwa huduma ya usafirishaji kati ya Morogoro na Dar es Salaam na baadae Dodoma kunatajwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo hapa nchini.
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli imeweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ili kukuza na kujenga uchumi jumuishi unaowawezesha wananchi kuondokana na umasikini kwa kujikwamua kiuchumi.