Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara Yatoa Rai kwa Wadau wa Sekta ya Utalii Nchini Kuendeleza Programu ya Royal Tour, Yagawa Vifaa vya Kujikinga na Uviko - 19
May 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael ameeleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kushirikiana vizuri na wadau wa Sekta ya Utalii katika kuendeleza Programu ya Royal Tour ili kuvutia watalii kutoka katika masoko mbalimbali duniani waje kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania.

Amesema Programu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni fursa ya Kimkakati ya kuitambulisha Tanzania Kimataifa,kuvutia uwekezaji nchini na kutangaza utalii.

Dkt. Francis Michael ameyasema hayo leo jijini Arusha alipokuwa akigawa vifaa vya kujikinga na janga la UVIKO- 19 kwa Wadau wa Sekta ya Utalii nchini.

Amesema Sekta ya Utalii nchini Tanzania inaendelea kuimarika baada ya athari za janga la UVIKO 19 kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuirejesha katika hali yake ya awali.

"Kipekee namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada mahususi alizozichukua za kuitangaza Tanzania Kimataifa kupitia programu maalum ya Royal Tour ambayo imeenda sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya UVIKO -19, ni ukweli usiopingika kuwa Royal Tour ni fursa ya kimkakati ya kuitambulisha Tanzania Kimataifa, kuvutia uwekezaji na kutangaza utalii" Amesisitiza Dkt. Francis Michael.

Ameongeza kuwa katika Mapambano dhidi ya Janga la UVIKO -19, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Mpango wa Maendeleo aliipatia Wizara ya Maliasili na Utalii fedha shilingi Bilioni 90.2 ambapo sehemu ya fedha hizo zimetumika kuimarisha Sekta ya Utalii katika maeneo mbalimbali.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara zenye urefu wa Kilometa 2,383.12 katika maeneo ya Hifadhi za Taifa, kujenga malango 14 ya kupokelea wageni katika maeneo ya hifadhi, Mapori ya Akiba, Tengefu na Misitu ya Hifadhi ya Mazingira Asilia.

Ameongeza kuwa Wizara imetenga maeneo ya uwekezaji na uendelezaji wa shughuli za utalii, kutoa mafunzo katika Sekta ya Utalii na Tasnia ya Ukarimu kwa wadau wa Utalii nchini, kuimarisha ulinzi na usalama wa watalii katika maeneo ya vivutio na kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Dkt. Francis Michael amebainisha kuwa taarifa za mwenendo wa Utalii zinaonesha kuwa katika kipindi cha msimu wa watalii mwaka huu Tanzania inatarajiwa kupokea idadi kubwa ya watalii na kuongeza kuwa matarajio hayo yanapaswa kwenda sambamba na maandalizi stahiki ya kupokea watalii hao na kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO -19.

Amesema kwa kutambua umuhimu huo Serikali imegawa imegawa vifaa vya kujikinga na janga la UVIKO -19 kwa wadau hao kupitia vyama vidogo vya watalii 10 vinavyojumuisha wafanyabiashara wadogo wadogo 16,056 ili kuhakikisha afya za wananchi na watalii zinalindwa ipasavyo na kuendelea kujenga imani kwa watalii kuwa Tanzania ni nchi salama ya kutembelewa.

Vifaa hivyo vinajumuisha barakoa 140,000 na vitakasa mikono 14,285.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi