Na Daudi Manongi,Mwanza
Wananchi wa Jiji la Mwanza pamoja na waliotoka katika Mikoa mbalimbali na wale wa Afrika Mashariki wameendelea kutembelea banda la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na mabanda ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ambapo kwa nyakati tofauti wamepongeza huduma na elimu inayotolewa na wataalam wa Wizara na Taasisi zake hususan juu ya Majukumu ya Wizara hiyo yanayogusa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.Pongezi hizo wamezitoa katika viwanja vya Rock city mall jijini Mwanza ambao maonyesho ya 21 ya wajasiriamali wadogo na wa kati yanaendelea ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Wizara hiyo Bi.Hanna Churi kutoka Singida amesema kuwa elimu aliyoipata kutoka kwenye banda la Wizara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu namna Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unavyosaidia kupitisha na kusafirisha mawasiliano ya aina zote, ikiwemo huduma za intaneti, taarifa mbalimbali, picha za video na kuongea kwa simu kwa usikivu madhubuti.
“Kwa kweli nimefuraishwa sana na huduma mnazotoa katika maonyesho haya nime elimika vya kutosha kwa kutembelea banda lenu na mmefanya jambo jema kwa kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi ” amesema Churi.
Kwa upande wake Bi Emilia James kutoka Arusha amesema amefurahishwa na taarifa alizopata kuhusu namna Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unavyofanya kazi na kufahamu jinsi gani utawanufaisha wananchi katika maeneo yao.
Aidha kwa upande wa Ibrahim Chorwa Mkazi wa Mwanza amesema amevutiwa na majukumu mbalimbali ya Idara ya Habari-MAELEZO ikiwemo kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera, Mipango na Miradi ya Maendeleo vinavyotekelezwa na Serikali kwa wananchi na kuipongeza Idara iyo kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Maonyesho ya 21 ya wajasiriamali wadogo na wa kati wa Afrika Mashariki yalianza tarehe 2 Disemba na yatamalizika tarehe 12 Disemba 2021 jijini Mwanza