Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara Nne Zaunda Kamati Mzee Kisangani Kuwa Bilionea
Mar 30, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_51902" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiongoza wajumbe wa Wizara nne kwa ajili ya kumsaidia Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani ambae ni mjasiriamali kutoka wilayani Ludewa aliyeanzisha kiwanda cha kutengeneza zana za madini ya chuma.Issa Mtuwa – Dodoma[/caption]

Kamati hiyo iliyoundwa Machi 30, 2020 yenye  wataalam 9 kutoka Wizara ya Madini,  Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeundwa ili kumsaidia Mjasiriamali wa miaka 60 kutoka Mkoa wa Njombe wilayani Ludewa, Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani ili kutimiza ndoto yake ya kuwa bilionea baada ya kubuni kiwanda kinachotengeneza zana zinazotokana na madini ya chuma.

Akifungua kikao hicho, Waziri Biteko amewaeleza wajumbe hao kuwa lengo ni kujadili namna ya kumsaidia Mzee Kisangani kwenye kila hatua kutoka mahali alipo ili ikibidi awe bilionea.

Ameongeza kuwa, mzee Kisangani hajui kusoma wala kuandika lakini ameonyesha kitu ambacho kama Serikali inahitaji kumsaidia kwa kila hatua anayohitaji.

Biteko amesema, alipokuwa ziarani mkoani Njombe kuanzia Machi 13-16, alitembelea kiwanda chake ambapo kwa namna kilivyo, lakini kinatengeneza zana mbalimbali za chuma kama vile, mapanga, fyekeo, visu, majembe huku akiwa amewaajiri watu 30.

[caption id="attachment_51901" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye sweta jeupe) na wananchi mbalimbali wakimsikiliza Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani alipomtembelea kwenye kiwanda chake cha kutengeneza zana mbalimbali[/caption]

Kutokana na uthubutu na juhudi alizonazo. Waziri Biteko akiwa ziarani katika eneo hilo aliahidi kukutana na Mawaziri wote wanaohusiana na shughuli zake ili kujadili namna ya kumsaidia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu akichangia namna ya kumsaidia, amesema wizara yake kupitia NEMC itahitaji andiko (Bussines Plan) na kwamba wataalam wa eneo hilo watasimama ipasavyo kumsaidia Mzee Kisangani kufikia ndoto yake. Wakati Zungu akihitaji andiko, Biteko amesema tayari Chuo Kikuu cha Mzumbe walishajitolea kumuandikia andiko la biashara (Business Plan) ya kiwanda chake.

Naye Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI, Mwita Waitara amesema kila mkoa ulipewa agizo la kuandaa maeneo ya uwekezaji hivyo Mkuu wa Mkoa huo atatoa eneo maalum kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha Kisangani kwenye eneo lililotengwa.

Kwa upande wake, Naibu wa Viwanda na Biashara Mhandisi, Stella Manyanya amesema kumekuwa na changamoto nyingi za kuwasaidia watu wenye ubunifu hususani kutokana na vipengele vilivyowekwa kisheria suala ambalo huwakatisha tamaa. Amesema wizara yake kupitia NDC, SIDO na TIRDO kila taasisi itatoa mtaalam kwa ajili ya kumsaidia mjasiriamali huyu ili afikie malengo.

Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi amesema mara baada ya kusoma taarifa za ziara ya Waziri wa Madini kupitia vyombo vya habari alituma wataalam kwenda kiwandani hapo na kuona namna gani ya kumsaidia ili kuzalisha chuma na kuongeza uwezo wa uzalishaji.

Waziri Biteko ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, amesema kwa kuwa tunataka kuona matokeo ya huyu Mzee kutokana na nguvu za Serikali ndipo iliamriwa kuundwa kwa kamati ya wataalam wa aina mbalimbali ambao ni wizara/taasisi kwenye mabano, Wilfred Machumu (Tume ya Madini), Issa Mtuwa (Wizara ya Madini), Abbas Mruma (GST), Prof. Silvester Mpanduji (SIDO), Prof. Madundo Mtambo Mkumbukwa (TIRDO), Dr. Yohana Mtoni (NDC), Anorld Mapinduzi (NEMC), Leo Mavuka (TAMISEMI), na Dr. Hellen (Chuo Kikuu Mzumbe.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi