Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ya kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari katika ya majiji makubwa nchini, ikiwemo kuanzisha reli za ndani ya majiji ili kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mhe. Mwigulu amesema hayo leo Juni 4, 2026 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Mhe. Haran Sanga aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kupunguza msongamano wa magari katika Majiji nchini.

Amesema tayari Serikali imechukua hatua mbalimbali za kupunguza msongamano kwa kuongeza barabara za ndani kwa kiwango cha lami na kujenga barabara za mzunguko (Bypass) ili magari yasiyo na ulazima wa kuingia katikati ya miji yaweze kutumia njia mbadala.
“ Serikali inaendelea kuchukua hatua kuondoa misongamano katika miji yetu inayokua. Baadhi ya miradi imekamilika katika Jiji la Arusha, pia ujenzi unaendelea katika mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa, Mwanza, Mbeya na Ruvuma. Amesema.

Mhe. Mwigulu ameeleza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kupunguza msongamano katika majiji yanayokua kwa kasi.
Kwa upande wa reli za ndani ya majiji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya awali ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu katika baadhi ya maeneo, sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya Reli ya Kisasa (SGR) inayounganisha Mikoa mbalimbali nchini.

Amevitaja vipande vinavyoendelea kujengwa kuwa ni Dodoma–Tabora, Tabora–Isaka, Isaka–Mwanza, Tabora–Kigoma na Kaliua–Mpanda akibainisha kuwa miradi hiyo itafungua fursa zaidi za kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali iko tayari kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika utekelezaji wa reli za ndani ya majiji.