Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kupitia uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika sekta ya fedha nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 2, 2026 na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akiwasilisha bungeni taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri Omar amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kufungamanisha mifumo ya kifedha ya Serikali na taasisi nyingine muhimu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa watumishi wa umma, wastaafu na wananchi kwa ujumla.
“Katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ilipanga kufungamanisha mfumo wa uhasibu Serikalini (MOSIP) na mfumo wa bima ya afya, mfumo wa malipo ya wastaafu wanaolipwa na Hazina (TPPS), mfumo wa usimamizi wa wanachama wa PSSF pamoja na mifumo ya benki za biashara ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi na wastaafu,” amesema Waziri Omar.
Mbali na hatua hizo amesema Serikali imeendelea na ujenzi wa mfumo wa pamoja wa kutoa ankara za malipo ya Serikali, ambao unatarajiwa kuimarisha usimamizi wa mapato yatokanayo na ada, tozo na huduma mbalimbali za umma.
Waziri Omar amesema mfumo huo utarahisisha ukusanyaji wa mapato, kupunguza gharama za kufanya biashara na kuchangia kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kufungamanisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma na mifumo ya taasisi mbalimbali ikiwemo benki za biashara, mifuko ya hifadhi ya jamii na mifumo ya ununuzi wa umma kwa lengo la kuongeza ufanisi, kasi na ubora wa huduma zinazotolewa.
Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Wizara ya Fedha ilifanikiwa kukusanya na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kutoka vyanzo vya ndani na nje kwa kiwango kikubwa, mafanikio yanayoelezwa kuchangiwa na maboresho yanayoendelea kufanyika katika mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha za Serikali.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika usimamizi wa fedha za umma yanasaidia kuongeza uwazi, kuimarisha uwajibikaji, kupunguza mianya ya upotevu wa mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika mifumo na teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma, kukuza mapato ya Serikali na kuhakikisha malengo ya maendeleo ya Taifa yanafikiwa kwa kasi na tija zaidi.