Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wilaya ya Kinondoni Yashika Kasi Uwekaji Anwani za Makazi
Apr 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho


 Yafikia asilimia 95 ya zoezi

Na Abubakari W. Kafumba, Kinondoni – Dar es Salaam

Zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi Wilaya ya Kinondoni limeendelea kwa ufanisi mkubwa tangu lilipozinduliwa rasmi kwenye wilaya hiyo tarehe 18 Februari, 2022. Kinondoni kati ya wilaya nyingine za Dar es Salaam imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutekeleza zoezi hilo kwa kasi ambapo mpaka sasa limefikia asilimia 95.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe ameeleza kuwa Kinondoni imekuwa na mwitikio mkubwa sana kwenye zoezi zima la Anwani za Makazi na ni chachu ya kuchochea maendeleo ya pamoja na binafsi.

Hili limewezekana kufuatia utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa Anwani za Makazi kuanzia ngazi ya chini ya Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Mitaa, Maafisa Tarafa, Mabaraza ya Madiwani, wataalamu wanaoendesha zoezi zima hadi katika ngazi ya kaya kwa wana-Kinondoni.

”Tulitaka wananchi waweze kufahamu na waweze kuitikia kwa hiari ili walichangamkie na walifurahie zoezi la Anwani ya Makazi. Zoezi linaendelea vizuri na tunafahamu umuhimu wake na tunajua kwamba hii ni moja ya fursa kubwa sana kwetu. Tumeshajipanga tayari na kazi ilishaanza muda mrefu. Tulianza kwanza kwa kutoa elimu ili wana-Kinondoni waweze kuelewa umuhimu wake kwa Maisha yetu ya kila siku,”ameeleza Mhe. Gondwe.

Kwa upnde wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Hanifa Suleiman Hamza amesema kuwa Manispaa hiyo ya Kinondoni yenye Postikodi namba 14000 ambayo imeundwa na Tarafa 2, kata 20 na mitaa 106 ina takriban ya watu 926,681 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na idadi inatarajiwa kuongezeka kufikia watu 1,514,000 ifanyikapo sensa ya mwaka huu 2022/23.

“Mpaka sasa Wilaya yetu ina takriban nyumba 135,942. Kati ya nyumba hizo nyumba 45,070 sawa na asilimia 33.1 zimeshawekwa kwenye mfumo. Kwa ujumla nyumba zote za Kinondoni zimefanikiwa kupewa namba za nyumba ambapo wakusanya taarifa wameshapita kwenye kila kaya kukusanya taarifa za wakazi wote hivyo zoezi zima la uandikishaji limefikia asilimia 95 mpaka sasa,” ameeleza Bi. Hanifa.

Zoezi hili la uwekaji wa Anwani za Makazi katika Wilaya ya Kinondoni limeleta fursa nyingi kwa wakazi wake ikiwemo upatikanaji wa ajira za wakati ambapo takriban vijana 250 wameajiriwa kwa ajili ya kukusanya taarifa za wakazi katika maeneo mbalimbali na waunda vyuma ambao wanatengeneza nguzo na vibao vya majina ya mitaa.

Uwepo wa zoezi hili umeendelea kuboresha ufanyaji biashara hasa kwa wale wanaojishughulisha na biashara za mtandaoni. Kwa wale wanaonunua bidhaa wanafikiwa kwa haraka bila kupotea na wale wanaouza wameendelea kufanya biashara kwa kuaminika zaidi na wateja wao kwa kuwa wanajulikana mahali walipo. Aidha, zoezi hili limeendelea kurahisisha upelekaji wa huduma mbalimbali kwa wateja ikiwemo huduma za afya, umeme, maji na huduma za uokoaji endapo janga linatokea.

Dunia sasa inakwenda kidijiti na nchi inaenda kuwa kijaganjani kupitia zoezi hili ambalo linaendelea kikamilifu. Matarajio ni kufikia Tanzania ya kidijiti ambapo watu, huduma au bidhaa hazikwami ili kama taifa tuweze kwenda sawa pamoja kuanzia ngazi ya chini ya kaya mpaka kitaifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi