Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wenza wa Viongozi Wagusa Mioyo ya Waathirika Hanang’
Dec 19, 2023
Wenza wa Viongozi Wagusa Mioyo ya Waathirika Hanang’
Wenza wa Viongozi wa Serikali, kupitia kikundi chao cha Ladies of New Millennium Group wakitoa msaada wilayani Hanang' baada ya maafa yaliyotokea Desemba 3, mwaka
Na Mwandishi wetu-Hanang’

Wenza wa Viongozi wa Serikali, kupitia kikundi chao cha Ladies of New Millennium Group, wametembelea maeneo yaliyoathiriwa na maafa yaliyotokea Desemba 3 mwaka huu wilayani Hanang’ Mkoa wa Manyara na baadae kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa hayo.

Akiongea mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na kukabidhi misaada, Mkuu wa msafara huo, Mama Mary Majaliwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa nguvu kubwa aliyoielekeza katika kuwasaidia waathirika wa maafa ili kuhakikisha kuwa maisha ya waathirika hao na maeneo yaliyoathiriwa yanarejea haraka katika hali ya kawaida.

“Tunapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia na Serikali yake kwa juhudi kubwa zinazoendelea kufanyika katika mji wa Katesh, lakini pia kwa upendo wake mkubwa kwa wananchi wa Hanang’ na hata kukatisha ziara yake ya kikazi kwa ajili ya wananchi hawa”, ameeleza Mama Mary Majaliwa.

Mama Majaliwa ambaye ni Mke wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wananchi wa Hanang’ na wale walioathirika na maafa kuwa na mshikamano katika kipindi hiki na kuwasisitiza kuendelea na shughuli zao na kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule mara tu zitakapofunguliwa mwezi Januari mwaka 2024.

Kwa upande wake, Bi. Marina Juma ambaye ni Mke wa Jaji Mkuu wa Tanzania, ametoa wito kwa wakina mama wengine kuguswa na athari za maafa hayo na kujitolea chochote watakachoweza ili kusaidia waathirika wa maafa hayo.

Mke wa Hayati Mzee Rashid Mfaume Kawawa, Mama Asina Kawawa ameelezea kuguswa na namna Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoshughulikia suala la maafa ya Hanang’. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa wema na busara zake kwa kuhakikisha anawajengea nyumba wale wote waliopoteza nyumba katika maafa haya. Mheshimiwa Rais ametuhamasisha sana kikundi chetu, nasi tukaona tuje kusaidia waathirika”, ameeleza Asina Kawawa.

Akiongea baada ya kupokea misaada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema kuwa kwa sasa serikali inaendelea kurejesha mji wa Katesh na maeneo mengine yaliyoathirika katika hali yake ya kawaida ikiwemo miundombinu ya barabara, maji na pia kusaidia kutoa tope yaliyoingia katika nyumba za watu.

“Wananchi wa Hanang’ hususani maeneo ya Katesh, Gendabi na Jorodom wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa msaada mkubwa ambao ameutoa”, amesema Mhe. Sendiga.

Kundi la New Millenium ambalo linaundwa na wake wa Viongozi limetoa misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa, ikiwemo mabegi ya shule 250, viatu vya shule jozi 216, madaftari 500, madaftari makubwa 144, kalamu za risasi boksi tano, sare za shule 200, chupi za watoto 600, fulana 170 kanga zaidi ya 100, vitenge 40, shuka 105 na blanketi 125. Vitu vingine ni mashati, magauni, suruali, mitandio, vyandarua, vyombo vya chakula pamoja na mchele kilo 450.

Maporomoko ya tope lililoambatana na mawe na magogo yalitokea Desemba 3, 2023 katika wilaya ya Hanang’ na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi 139 pamoja na uharibifu wa nyumba, mali na miundombinu mbalimbali ya maji, umeme, barabara na pia kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi hususan katika mji wa Katesh pamoja na vijiji vya Gendabi na Jorodom.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi