Na mwandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene amepongeza vijana waliojiunga katika Kikundi cha Kisima umoja Vijana kwa moyo wao wa uzalendo wa kuchangia madawati katika shule ya Msingi Kisima.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu (Mb), Mhe. George Simbachawene katika ziara yake ya kutembelea na Kuzungumza na wananchi katika Jimbo lake la uchaguzi Kibakwe Halmashauri ya Mpwapwa.
“Vijana wameweza kuchangia madawati 14 yenye thamani karibu ya Shilingi milioni moja, ni jambo kubwa na vijana wengine igeni mfano wa vijana hawa.”Alisema Waziri Simbachawene.
Wamekumbuka nyumbani wameona wadogo zao wakae mahali pazuri kwa kuamua kutengeneza madawati, na umoja wao ni wa watu ambao hawana kitu lakini ni umoja ambao una dhamira.
“Jambo la msingi katika maisha ni kuwa na dhamira na jambo lako, kwa sababu Mungu anabariki mipango, Mungu anabariki dhamira,” alisema Waziri.
Kwa niaba ya viongozi Serikalini na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi naomba niwashukuru sana kwa tendo hili linaloonesha umoja ni nguvu.
Akisoma taarifa ya Kikundi cha Kisima Umoja Vijana, mbele ya Waziri Bwn. Kepher Mdachi amesema malengo yao ni kuendelea kusaidia jamii yetu na ambazo ziko ndani ya uwezo wa kikundi hicho.
“Kutoa hamasa kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu, kutoa elimu kwa jamii kwa kuwafikia wazazi na walezi ili kuwahamasisha umuhimu wa elimu kwa vijana wao.”
Aidha, kikundi hicho kimelenga kujenga taasisi imara itakayolenga kusaidia jamii na kufanya jambo la kijamii kila mwisho wa mwaka ikiwa ni pamoja na kusaidia sekta ya afya kwa kuchangia vifaa tiba vyenye uhitaji wa haraka.
“Madawati haya yamepatikana kutokana na utaratibu wa kutoa ada kwa kila mmoja kuanzia Shilingi 2,000 kadiri anavyojaliwa, na hufanywa kwa hiari. Tumezidi kuwa wamoja pale tunaposikia changamoto za kijamii ikiwa ni pamoja na kusaidiana sisi wenyewe kama mmoja wanakikundi amepata shida,” alisema Mdachi.