Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye leo Aprili 11, 2022 ameanza ziara ya siku moja leo ya kukagua utekelezaji na kuhamasisha zoezi la Anwani za Makazi katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha .
Akizungumza mapema leo katika Uwanja wa Ndege jijini Dodoma, Waziri Nape amesema kuwa ziara hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanakuwa na Anwani za Makazi ikiwa ni lengo la Serikali kuhakikisha kuwa kunakuwepo na anwani za kitaifa ambazo zitaainisha makazi, mahali zilipo Ofisi na maeneo ya biashara.
“Operesheni hii iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tamzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambayo kwa sasa imefikia takribani asilimia 69 ina lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata Anwani za Makazi ili kurahishisha ufikishaji wa huduma mbalimbali za jamii na biashara kwa walengwa” alisema Waziri Nape.
Aliongeza kuwa licha ya kuwa zoezi hilo limefanikiwa katika baadhi ya mikoa kama Lindi na Ruvuma bado kumekuwepo na mikoa michache ya Tanga na Dar Es Salaam ambayo haijafanya vizuri na hivyo Serikali inajipanga kuhakikisha mikoa yote inafanikiwa katika zoezi hilo.
“Ndio maana tumeamua kutembelea maeneo ambayo zoezi hili linatekelezwa ili kusaidia kuongeza utaalamu katika mikoa yenye changamoto ya utekelezaji, lakini pia kuangalia sababu zilizosaidia mikoa mingine kufanikiwa zaidi na hivyo kuzitumia kusaidia mikoa ambayo inahitaji msaada zaidi” Alisisitiza Waziri Nape.
Operesheni hiyo maalum ya kukagua utekelezaji na uhamasishaji wa zoezi la Anwani za Makazi inatarajia kufanyika nchi nzima ambapo Aprili 13, 2022 ziara hii itaendela katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi na Aprili 14, 2022 katika mkoa wa Pwani.