Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Nape: Natoa Siku 14 Maafisa Habari Kuhuisha Tovuti za Serikali
May 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kuhuisha taarifa za Serikali kwenye tovuti za Serikali na mitando ya kijamii ili wananchi waweze kupata taarifa na kujua kinachoendelea kuhusu Serikali yao.

Akizungumza leo jijini Tanga wakati akifungua Kikao cha 17 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali, Waziri Nape amesema kuwa Maafisa Habari wa Serikali ni daraja linalorahisisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, hivyo ni muhimu kutimiza wajibu wao kwa kuwa na taarifa sahihi za Serikali na kwa wakati katika tovuti za Wizara au Taasisi zao.

“Natoa siku 14 kuanzia Mei 14, 2022, kila tovuti ya Serikali na mitandao ya kijamii iwe na taarifa za Serikali zinazoendana na wakati kuhusu utekelezaji wa Sera au miradi mbalimbali ya Serikali, Afisa atakayeshindwa kutekeleza hili tutaachana nae”, amesema Mheshimiwa Nape

Aidha, akiwa katika kikao hicho Waziri Nape ameiagiza Idara ya Habari – MAELEZO kuandaa mfumo utakaowezesha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano nchini kupatiwa mafunzo kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini ili waweze kuwa na uelewa na kuweza kuisemea miradi hiyo, kuandaa mfumo wa Maafisa Habari kujadiliana masuala mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na kuwa na mfumo wa kupima utendaji kazi wa Maafisa hao.

Katika hatua nyingine, Waziri Nape ameahidi kutatua changamoto ya uhaba wa Maafisa Habari katika ngazi ya Wizara na Halmashauri ili kuhakikisha Serikali ina wataalamu wa kuisemea katika ngazi hizo.

“Nawaahidi hili liko ndani ya uwezo wangu la kusaidia kupata Maafisa habari katika Mikoa ya Lindi, Manyara, Mbeya na Tabora na Mikoa ya Dodoma, Kigoma na Geita ambayo Maafisa Habari wake wamekuwa Wasaidizi wa Wakuu wa Mikoa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Kikao Kazi hicho kitaandaa mkakati na kujifunza namna ambavyo dunia itahabarika kupitia Tanzania na kufikisha ujumbe wa maendeleo na namna ya watu kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Pia, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa kuwa lengo la kikao kazi hicho cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini ni kujengeana uwezo wa namna bora ya kuisemea Serikali na kuwa atahakikisha maagizo yote yaliyotolewa yanatekelezwa ili kutimiza jukumu hilo kwa ufanisi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi