[caption id="attachment_6637" align="aligncenter" width="621"] Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza Mkataba wa Ubia baina ya TBC na Kampuni ya Startimes ambaye pia ni Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi[/caption]
Na. Judith Mhina
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameiongezea muda wa siku kumi, Kamati ya kuchunguza mkataba wa ubia kati ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na Kampuni ya StarTimes.
Akiongea kwa niaba ya Waziri Mwakyembe, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Hassan Abbasi, amesema Kamati ilipewa hadidu za rejea nane katika kuchunguza mkataba huo lakini kutokana na umuhimu wa kazi hiyo, Kamati iliona kuna mambo yanahitaji kuchunguzwa kwa kina na hivyo kuomba muda zaidi.
“Kamati imefanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa lakini tumeomba kuongezewa siku kumi zaidi na Waziri karidhia kwa sababu kuna mambo muhimu Kamati inahitaji kuyafanyia kazi kwa kwa kina kwa maslahi ya Tafia,” ameeleza Dkt. Abbasi.
Julai 15 mwaka huu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe aliunda Kamati kufuatilia mkataba husika kutokana na kutopatikana kwa faida kwa kipindi cha miaka saba.
Pamoja na Mwenyekiti wa Kamati wajumbe wengine wanaounda Kamati hiyo kwa upande wa Tanzania ni Bw. Kyando Evod kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Frederick Ntobi na Mhandisi Adrew Kisaka wote kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Bw. Mbwilo Kitujime kutoka Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Aidha, wajumbe wengine watano wanatokea upande wa China.
Kabla ya kuunda Kamati hiyo, Waziri Mwakyembe alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya StarTimes kutoka China, Xinxin Pang kujadiliana kwa kina juu ya mkataba huo ambapo katika majadiliano hayo walikuwepo wafanyakazi wa Wizara hiyo akiwemo Katibu Mkuu, Profesa Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Abbasi.
Sakata hili la kuchunguza mkataba huo limetokana na ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kutembelea ofisi za TBC mwezi Mei mwaka huu na kuonesha kukerwa na kutopatikana kwa faida kwa kipindi cha miaka saba na kuagiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki.