Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mwakyembe Aikabidhi Bendera Timu ya Azania tayari kushiriki Kombe la Standard Chartered Nchini Uingereza.
May 17, 2017
Na Msemaji Mkuu

 

Na: Genofeva Matemu – WHUSM.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe ameikabidhi Bendera ya Taifa Timu ya Mpira wa Miguu ya Azania inayoenda kuiwakilisha Tanzania katika Michuano ya kombe la Standard Chartered nchini Uingereza.

Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo Mhe. Mwakyembe amewataka vijana wa Timu hiyo kukumbuka kuwa ni muda wa kuonyesha uwezo na vipaji walivyonavyo na kuvitumia kuiletea nchi heshima na kuitangaza katika mataifa mengine Duniani.

“Kuwa mabingwa na kuweza kuiwakilisha Afrika Mashariki kuwania kombe la Standard Chartered mmeonyesha uwezo wa hali ya juu, naamini mtatumia uwezo huo  kufanya vizuri zaidi katika michuano hiyo.”Amesema Mhe. Mwakyembe.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Standard Chartered Tanzania Balozi Ami Mpungwe amesema kuwa Timu ya Azania ina uwezo kwani imefanya vizuri hapa nyumbani katika  michuano ya kitaifa na kanda ya Afrika Mashariki ili kuhakikisha  wanapata ubingwa ambao umewawezesha kusonga mbele na kuitoa  Kenya ambao ndio mabingwa watetezi.

 

Naye Balozi wa Uingereza Tanzania Mhe. Sarah Cooke amewataka wachezaji hao  kupambana  kwa ari na uwezo  mkubwa na kanda nyingine za nchi za Afrika pamoja na mabara mengine wakiwa na lengo la kurejea nchini na ushindi ili kuitangaza nchi yetu kupitia kombe la Standard Chartered.

Michuano ya kuwania kombe la Standard Chartered inahusisha nchi zote ambazo Benki ya Standard Chartered ina matawi ambapo kwa Tanzania Timu ya Azania inashiriki na mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Mei 21 mwaka huu katika viwanja vya Anfield nchini Uingereza.

     

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi