Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu: Serikali Imeshalipa Bilioni 222, Itanunua Korosho Yote Itakayohakikiwa
Dec 30, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema jumla ya shilingi bilioni 222 zimelipwa na Serikali kwa wakulima wa zao la korosho na kuwataka wakulima wawe na subira.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Nandagala ‘A’ baada ya kufungua ofisi ya CCM kata ya Nandagala Mkoani Lindi.

Amesema kuwa wakulima walioanza kulipwa ni wale wenye kilo zisizozidi kilo 1,500 na wale wenye kilo zaidi ya 1,500 na kuendelea Serikali inaendelea na uhakiki kisha watalipwa.

"Fedha zipo, hakuna mkulima ambaye atapoteza haki yake wote watalipwa, tunaendelea na uhakiki kwa wale wenye korosho nyingi ili kubaini kama hawajanunua kangomba" ameongeza Waziri Mkuu.

Kauli hii ya Waziri Mkuu ni tofauti na taarifa za upotoshaji zinazonukuu baadhi ya mitandao, hivyo kwa kauli hiyo ya Waziri Mkuu msimamo wa Serikali unabaki ule ule kuwa korosho yote ya wananchi itakayohakikiwa itanunuliwa na Serikali na amewataka wananchi wasiwe na wasiwasi.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa, baadhi ya watu wamekutwa na kilo zaidi ya 1,500 na wameshindwa kuonesha mashamba yao ya mikorosho, hali inayodhihirisha kwamba amenunua kupitia kangomba.

Waziri Mkuu amefafanua kuna baadhi ya waliokutwa na korosho nyingi ikiwemo vijana wadogo ambao hawana uwezo kifedha, hivyo Serikali itahakikisha inawakamata watu wanaowatuma.

Amesema lengo la Serikali inayoongizwa na Rais Dkt. John Magufuli ni kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao, hivyo biashara ya kangomba lazima lidhibitiwe.

Mbali na hayo Waziri Mkuu amesema zoezi la ulipaji kwa wakulima wa korosho linaendelea hivyo kuwataka wakulima hao kuwa na subira.

Serikali iliamua kununua korosho zote za mwaka huu baada ya kubaini wafanyabiashara kuwa na nia ya kuwadhulumu wakulima wa zao hilo kwa kununua korosho hizo kwa bei ya chini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi