Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Awataka Viongozi, Watumishi wa Umma Kuepuka Ubadhilifu
Dec 11, 2025
Na Baraka Messa - MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Mwigulu Lameck Nchemba amewataka viongozi na watumishi wa umma, kufuata na kuzingatia maadili ya utumishi ili kupunguza mianya ya rushwa ambayo imekuwa kikwazo kwa utoaji huduma bora kwa jamii.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo novemba, 11, 2025 jijini Dodoma wakati wa kikao na viongozi na Watendaji wa Sekretarieti ya maadili kwa Viongozi wa Umma, Amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwenye masuala hayo ya usimamizi wa maadili ya utumishi wa umma.

Amesema moja ya jambo ambalo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amelisema mara nyingi ni suala linalohusu maadili ya viongozi pamoja na watumishi wa umma.

"Kukaa kwangu serikalini kuna mambo ambayo nimejifunza ambayo hayahitaji shule kuyajua, jambo la kwanza ninalolijua ni maeneo ambayo fedha ya umma huwa inaweza kupotea. Tunaweza tukaendelea kikamilifu kutengeneza suala la matamko kwa viongozi wa umma, tukatengeneza kikamilifu suala la sheria lakini uhalisia wake ikawa ukosefu wa maadili na rushwa vikaendelea hatutafanikiwa", amesema Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu ameyataja baadhi ya maeneo serikalini ambayo yanaongoza kwa mapungufu na kuagiza yafanyiwe kazi upya kuwa ni pamoja na kitengo cha manunuzi ambapo zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya serikali, fedha ya umma hutumika kwa ajili ya mikataba na manunuzi ambapo ameeleza kuwa eneo hilo lina matobo mengi ambayo hupelekea ubadhilifu wa fedha za umma.

Amesema eneo la manunuzi na mikataba huongoza kuwa na mianya ya rushwa na fedha za Serikali kupotea, hivyo kudai kuwa kuna sababu kubwa ya kufanya mabadiliko kwa kuweka watu wanaosimamia maafisa masuhuli na wanaosimamia kamati za wazabuni.

Maeneo mengine yenye mianya ya ubadhilifu aliyataja kuwa ni watumishi wanaotoa leseni za madini pamoja na vitengo vya ukaguzi na udhibiti .

Waziri Mkuu Dkt. Nchemba amemtaka Waziri wa Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete kubainisha maeneo ambayo yana rekodi za rushwa ili yapewe kipaumbele na kufanyiwa kazi upya.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi