Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Awataka Vijana Kutumia Mifumo ya Dijitali
Oct 11, 2024
Waziri Mkuu Awataka Vijana Kutumia Mifumo ya Dijitali
Waandamanaji wakipita mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2024 kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Oktoba 11, 2024.
Na Adelina Johnbosco

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amewaasa wananchi wote hasa vijana kutumia fursa ya kuwepo kwa mifumo ya dijitali hapa nchini kufanya shughuli zao hasa katika kujiingizia kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla ili kuendana na kasi ya  maendeleo duniani.

Amesema hayo jana Ijumaa Oktoba 11, 2024, wakati akizindua  wiki ya vijana kitaifa katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

‘’ Tayari Serikali yetu imeweka fursa na mikakati mbalimbali ya matumizi ya mifumo ya kidijitali  katika kuhakikisha shughuli zinatekelezwa kwa haraka na kwa wakati, maendeleo ya kidigitali yataboresha uchumi na yataleta maendeleo endelevu katika maisha yetu ya kila siku hasa kwa vijana. Vijana wa leo mnayo nafasi ya kujiendeleza kwa kuleta maendeleo ya taifa letu kwa kutumia ubunifu mbalimbali  digitali,’’ alisisitiza Mhe. Majaliwa

Aidha, alitaja dhumuni la maadhimisho ya wiki ya vijana kuwa ni pamoja na  kuonesha fursa zilizopo ninavyowanufaisha vijana, pamoja na kubadilishana uzoefu ‘’ Lengo la maadhimisho haya ni kutoa fursa kwa vijana kutambuana, kuelewa na kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye maendeleo ya taifa letu na Afrika kwa ujumla, kuja kupata falsafa ya maendeleo na historia ya waasisi wetu wa taifa,’’

Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa, amesema kwamba, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kupata maendeleo, ikiwemo; kuwapatia stadi na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira ili kupambana na changamoto ya ajira duniani, sekta binafsi kupokea vijana kwa ajili ya kuwapatia ujuzi kwenye maeneo mbalimbali tangu mwaka 2001 hadi sasa, kuwapeleka vyuo vya Serikali na binafsi ili kuwawezesha kujifunza, hii imetoa fursa kwa vijana kujiajiri na kuajiriwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, alibainisha jinsi Wizara yake inavyojikita katika uhamasishaji wa matumizi ya TEHAMA katika utendaji nchini, ‘’Wizara yetu kwa kushirikiana na wadau wetu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), tumeendelea kuwezesha idara mbalimbali na Serikali nzima kubuni mifano mbalimbali ambayo inaisaidia nchi yetu kutumia mifumo ya  kidigitali, tuendelee kuitumia ili kuweza kuyafikia malengo tuliyonayo kama nchi.’’

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita, ameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuwalea vijana na kuwaandaa kuwa wenye ujuzi, wabunifu na wazalendo ambao hivi sasa wanaipeperusha vyema bendera ya Tanzania, na kuahidi kuendelea kuyasimamia, kuyasikiliza na kuyatekeleza maelekezo yote ya Serikali ili kuhakikisha vijana wanawezeshwa katika kujiajiri na kuajirika katika Serikali na sekta binafsi ili kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi