Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Awaonya Wanaoiba Dawa Hospitali
Aug 10, 2017
Na Msemaji Mkuu

 Na: Tiganya Vincent, RS-Tabora

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewaonya wamiliki wa maduka ya dawa za binadamu na watumishi wa sekta ya afya wanaochukua dawa katika Hospitali za Serikali kwa ajili ua kuwahudumia wananchi na kuziweka katika maduka yao. Mhe. Majaliwa alitoa onyo hilo jana Wilayani Sikonge katika mkutano wa hadhara na wananchi katika Kiwanja cha TASAF. Alisema kuwa wizi wa dawa katika hospitali za Serikali umekuwa ukisababisha upungufu wa dawa katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mbalimbali za Serikali na kusababisha wananchi kuendelea kuteseka na maradhi kwa sababu ya kushindwa gharama za ununuzi wa dawa katika maduka ya watu binafsi. Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa aliwaonya watumishi wa afya na wamiliki wa maduka ya dawa wenye tabia ya kuiba dawa za Serikali kuacha mara moja na endapo watabainika kuendeleza wizi watachukuliwa hatua kali. Alisema kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kununua dawa kwa ajili ya matibabu kwa wananchi wake lakini kuna baadhi ya watumishi wa afya wasio waadirifu ambapo wamekuwa wakitorosha dawa na kuwauzia wamiliki wa maduka ya dawa na ksuababisha upungufu katika vituo vya Serikali. Waziri Mkuu alizitaka pia hospitali kuhakikisha zina dawa za kutosha ili kuepusha usumbufu kwa wananchi. Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameikabidhi Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tabora orodha ya watu wenye tabia ya kuwarubuni wakulima wa tumbaku na kununua katika mfumo ambao si rasmi kisheria (soko huria) na kinyonyaji ili wahojiwe. Alisema kuwa watu hao kwa muda mrefu ndio wamekuwa wakiwanyonya wakulima kununua tumbaku zao kwa vishanda na kuwa fedha ambazo zinazidi kuwakandamiza. “Nina majina ya watu ambao wamekuwa wakipita kwa wakulima na kununua tumbaku za wakulima kwa njia ya vishada ….huku wakiwanyonya kwa kuwapa fedha kidogo, nawataka waache mara moja.” Alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu. Aliongeza “leo siwataji majina yao lakini nakuachia Mkuu wa Mkoa ili wewe na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama muwaite na kuwahoji na kisha muwaonye wasiendelee na biashara hiyo, kama wanataka kuendelea na uuzaji wa tumbaku wahakikishe wanayopeleka sokoni ni ile waliolima wenyewe na sio ya kununua kwa wakulima” Aidha,Waziri Mkuu alitoa onyo kwa watumishi wa umma ambao wamekuwa na tabia ya kugonja wakulima walime tumbaku na wakisha kuvuna na kukausha wao wanakwenda kununua kwa ajili ya kuipeleka katika makampuni ya tumbaku. Alisema mtumishi hakatazwi kulima tumbaku lakini atakiwi kununua tumbaku kutoka kwa mkulima. Waziri Mkuu huyo aliwaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kukamata watu wote wanajihusisha na ulanguzi wa tumbaku ya wakulima na kuongeza kuwa watakamatwa wakiwa na tumbaku ya ulanguzi ichukuliwe pamoja na chombo cha usafiri kinachotumika kusafirishia. Alisema kuwa tumbaku yote inauzwa kupitia vyama vya msingi na kila mtu atauza tumbaku kwa kiwango alicholima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi