Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Awaonya Wachochezi
Jul 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewatahadharisha watu wote wenye tabia ya kutoa matamshi ya kichochezi nchini kuacha mara moja kwani Serikali itawashughulikia ipasavyo bila kujali bila ya kujali nyadhifa zao.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Bibi Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela mkoa wa Mbeya.

Waziri Mkuu alisema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.

Alisema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.

"Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo," alielezesha Waziri Mkuu.

Onyo hilo la Waziri Mkuu limekuja siku moja baada ya Serikali kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dkt. Hassan Abbasi kumuonya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu dhidi ya matamshi ya chuki, kejeli na uchochezi kuilenga Serikali kuwa inabana demokrasia nchini jambo ambalo si la kweli.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya Askofu wa Kanisa la Evarinjerical Brother Hood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli.

Amesema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi.

“Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo. Wanaofanya hivyo wasidhani kama wanamtukana Rais tu bali wanawatukana Watanzania wote waliomchagua wakiwemo viongozi wa dini.”

Pia aliwaomba wananchi kufanya maandalizi mapema kwa sababu wote ni wapitaji, hivyo waandae roho zao kwa kuacha kufanya dhambi na maovu yote ili wawe na mwisho mwema.

Vile Vile Waziri Mkuu amewaomba wananchi wote washirikiane kwa pamoja kumuombea Dkt. Mwakyembe na familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.

“Wajibu wetu sote ni kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema. Tunajua kwa sasa Dkt. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu, namuhakikishia kwamba hayuko peke yake kwani Serikali iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu.”

Naye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai alimpa pole Dkt. Mwakyembe huku akiitaka familia kuendelea kuwa na upendo kama ule uliokuwepo wakati wa uhai wa marehemu Bibi Linnah.

Kwa upande wake, Mtoto mkubwa wa marehemu, George Mwakyembe alisema anaamini mama yao, alijiandaa na kifo hicho kwa kuwa alikuwa mchamungu.

"Mama alikuwa na ratiba kila siku ifikapo saa nne usiku lazima afanye ibada, hivyo nina matumaini makubwa kupitia Uchamungu wake, Mwenyezi Mungu atamuweka mahala pema."

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi