Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Atembelea Mradi wa Kinyerezi II
Jul 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme Kinyerezi II, leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na.  Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametembelea mradi ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi II uliopo eneo la Kinyerezi Jijini Dar es Salaam leo na kusema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.

Baada ya kukagua mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, Waziri Mkuu alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, utakaowezesha kuendesha viwanda.

Alisema kuwa mkakati wa Serikali ni kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme ili Watanzania wapate umeme mwingi utakaosambazwa hadi vijijini kwa gharama nafuu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Wananchi wa Kinyerezi baada ya kutembelea mradi wa kuzalisha umeme Kinyerezi II, leo Jijini Dar es Salaam (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Tunataka tupate umeme wa kutosha ili viwanda vitakavyojengwa viwe na nishati ya uhakika na ya gharama nafuu. Ni wajibu wetu kuendelea kuimarisha utekelezaji wa miradi hii”, alieleza Maziri Mkuu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II, Mhandisi Stephen Manda alisema gharama za mradi huo ni dola milioni 344.

Meneja huyo alisema tayari mradi huo umefikia asilimia 66.32 ya ujenzi wake na sasa wako katika hatua mbalimbali za kukamilisha, ikiwemo ujenzi wa misingi ya mitambo na jengo la kuendeshea mitambo

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO Balozi, Dkt. James Nzagi, wakati alipoenda kukagua mradi wa kuzalisha umeme Kinyerezi II, leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Pia tunaendelea na ujenzi wa nguzo za kupokelea laini ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Kinyerezi I hadi Kinyerezi II, ambapo mtambo wa kwanza wa megawati 30 utawashwa ifikapo Desemba 2017 na kila mwezi tutaingiza megawati 30 katika gridi ya Taifa.”, alifafanua Injinia Manda.

Amesema miradi iliyopo katika eneo hilo ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Kinyerezi 1 (150MW), Kinyerezi I Extension (185MW) na Kinyerezi II (240MW).

Mhandisi Manda ameongeza kuwa mradi wa Kinyerezi 1 (150MW) ulikamilika Machi 2015 na miradi mwili ya Kinyerezi 1-extension na Kinyerezi II inatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akiongea na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, wakati alipotembelea mradi wa kuzalisha umeme Kinyerezi II, leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Aliitaja miradi mingine inayotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ni wa Kinyerezi III (600 MW) na Kinyerezi IV utakaozalisha (450 MW).

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, alisema mradi huo umewanufaisha wananchi wengi wa eneo hilo.

Alisema hadi sasa wananchi 100 wa eneo la Kinyerezi wameajiriwa katika miradi hiyo ambapo ni sawa na asilimia 40 ya watumishi wote.

Bi. Sophia alisema mbali na ajira pia wananchi wa eneo hilo watanufaika kwa kuboreshewa huduma mbalimbali za kijamii katika eneo hilo zikiwemo za maji na elimu ambapo shule tano zimeahidiwa kupatiwa madawati.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi