Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Atembelea Kambi ya Serengeti Boys
Apr 08, 2019
Na Msemaji Mkuu

*Asema Watanzania wana matumaini makubwa kwao, waongeze bidii,

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 na kuwaeleza kuwa Watanzania wana matumaini makubwa dhidi yao, hivyo waongeze bidii.

Alitembelea kambi hiyo ya Serengeti Boys iliyoko katika jiji la Kigali nchini Rwanda. Waziri Mkuu alikwenda Rwanda Aprili 7, 2019 kumuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye kumbukumbu za miaka 25 ya mauaji ya Kimbari.

Akizungumza na wachezaji hao jana (Jumapili, Aprili 8, 2019) Waziri Mkuu aliwataka vijana wanaounda timu hiyo ya Serengeti Boys wahakikishe wanafanya mazoezi ya kutosha ili waweze kushinda mechi zinazofuata.

“Watanzania wana matumaini makubwa dhidi yenu nasi tunazidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu muweze kuibuka na ushindi katika michezo yenu iliyobakia itakayowawezesha kushiriki mashindano ya kombe la dunia.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza timu hiyo ya Serengeti Boys kwa namna wanavyoitangaza nchi kimataifa kupitia kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki na kuibuka na ushindi.

Waziri Mkuu alisema endapo timu hiyo ya Taifa ya vijana ya Serengeti Boys itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia huko nchini Brazil kwa vijana wa umri wa miaka 17.

Kwa upande wao, wachezaji na uongozi wa timu ya Serengeti Boys walimkabidhi Waziri Mkuu kombe walilolipata baada ya kuichapa timu ya Rwanda katika mashindano maalumu kwa ajili ya kujiandaa na AFCON-U17.

Mashindano hayo maalumu ya Kimataifa yalishirikisha timu za umri wa chini ya miaka 17 kutoka nchi tatu ambazo ni Tanzania, Cameroon na wenyeji Rwanda, ambapo Serengeti Boys ilishinda mabao mawili kwa moja dhidi ya Cameroon na kutoka sare ya mabao matatu kwa matatu na Rwanda.

Pia, wachezaji hao wamemuahidi Waziri Mkuu kwamba watajitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha wanaibuka na ushidi katika mechi zilizobakia ili waweze kushiriki kombe la dunia. “Hatutawaangusha Watanzania.”

Awali, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mheshimiwa Balozi Ernest Mangu pamoja na maofisa wa ubalozi na Watanzania waishio Rwanda kwa kuendelea kuipa moyo Serengeti Boys.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, APRILI 9, 2019.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi