Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya wawe wabunifu na waandae miradi ya kimkakati ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo.
Ametoa wito huo leo (Jumatano, Februari 28, 2024) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Utegi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Usogo, wilayani Rorya, mkoani Mara.
“Nimepokea maombi ya Waheshimiwa Wabunge juu ya haja ya kuwa na soko kule mpakani na stendi kubwa hapa Utegi. Halmashauri mnayo dhamana ya kujenga kituo cha mabasi na miradi mingine ya kimkakati, ni kitu kizuri ili mradi mpange jinsi ya kukusanya mapato,” amesema.
“Ninawaagiza muwe wabunifu kwenye Halmashauri yenu. Andaeni andiko na mnaweza kuamua kulipeleka TAMISEMI ambako wana mfuko maalum na kama wakiridhika na andiko lenu wanawapatia mkopo. Au mnaweza kwenda Benki ya TIB ambako mtawaeleza jinsi mtakavyolipa kulingana na makusanyo,” amesema.
Kuhusu afya, Waziri Mkuu amewaeleza wananchi hao kuwa alienda kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Halmashauri hiyo ambako zilitolewa shilingi bilioni 3.5. “Hospitali hizi zinapaswa kuwa na majengo 27, ninyi mmeanza na majengo 16 ambapo saba yamekamilika na tisa yanaendelea kujengwa.”
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliamua kuwe na hospitali za Halmashauri badala ya kutegemea hospitali za wilaya peke yake. “Kwa maana hiyo kama kuna Halmashauri mbili, kila moja itakuwa na hospitali yake na zote zinajengwa kwa hadhi ile ile kama ya hospitali ya wilaya.”