Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshiriki ufunguzi wa mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM).
Mheshimiwa Majaliwa ameshiriki mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo wa siku mbili umeanza leo Ijumaa, Januari 19, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Ruwenzori, Kampala nchini Uganda.
Katika mkutano huo, Rais wa Uganda alikabidhiwa rasmi uenyekiti wa kundi hilo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Cuba Miguel Mario Diaz-Canel Bermudez.
Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan mwezi Oktoba, 2019. Mkutano huo haukuweza kufanyika tangu mwaka 2019 kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 lililoikumba dunia.
Awali, Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museven akizungumza baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa umoja huo aliahidi katika kipindi cha uongozi wake atatoa ushirikiano wa kutosha kwa mataifa yanayounda umoja huo ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanafikiwa.
Pia, Mheshimiwa Rais Museveni aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa nchi za Afrika hazina uhaba wa chakula kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
“Afrika ina kila kitu, sisi tunachotaka kutoka kwa nchi nyingine ikiwemo zilizoendelea, msimamo wetu ni kuwa dunia isimame kwenye changamoto za kawaida za binadamu na ustawi wa biashara.”
Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na uchumi wa kidijiti.
Umoja huo ulianzishwa wakati wa enzi za vita baridi ili kusaidia nchi wanachama wake kutoka mabara ya Asia, Afrika na Latin Amerika kuondokana na ukoloni ili kuweza kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijamii.