Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa amewasili leo Januari 18, 2024 nchini Uganda akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 - 20 Januari, 2024.
Pia, Mheshimiwa atamwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia katika mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77+China utakaofanyika tarehe 21-22 Januari, 2024, Kampala – Uganda.
Ujumbe wa Waziri Mkuu katika Mikutano hiyo utajumuisha viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba.
Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan mwezi Oktoba, 2019. NAM ni umoja wa nchi na Serikali 120 zenye msimamo wa sera ya kutofungamana na upande wowote.
Umoja huo ulianzishwa wakati wa enzi za vita baridi ili kusaidia nchi wanachama wake kutoka mabara ya Asia, Afrika na Latin Amerika kuondokana na ukoloni ili kuweza kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Akiwa nchini Uganda Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Kundi la G77 na China kuanzia tarehe 21-22 Januari, 2024. Mkutano huo unaotarajiwa kushirikisha nchi wanachama wapatao 134.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Januari Makamba amesema kuwa katika mkutano huo kutakuwa na ajenda muhimu zitakazojadiliwa na kuamuliwa na Wakuu wa Nchi.
“Katika mkutano NAM kutakuwa na maazimio mahususi yanayohusu masuala ya maendeleo ya uchumi, kijamii, ajira, ushirikiano wa kikanda na kimataifa, amani na usalama na masuala mengine yanayohusu nchi hizi zisizofungamana na upande wowote.”
Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na uchumi wa kidijiti.
Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni ndiye mwenyekiti wa mkutano huo na anatarajiwa kukabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Kundi hilo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Miguel Mario Diaz-Canel Bermúdez.