WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mkoa wa Lindi mwaka huu.
Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli imefanya maboresho makubwa kwa sekta ya eilimu nchini ikiwa ni pamoja na kufuta michango yote ya hovyo iliyokuwa ikiwakera wazazi na walezi.
Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Jumapili, Novemba 18, 2018) katika mkutano wa kuwapongeza walimu wa wilaya ya Ruangwa na baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu. Aliongeza kuwa matokeo ya mwaka jana halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ilishika nafasi ya tano kimkoa na kitaifa ilikuwa nafasi ya 141, ambapo kwa mwaka huu imepanda na kuwa nafasi ya kwanza kimkoa na kitaifa kuwa nafasi ya 84.
Kufuatia matokeo hayo mazuri Waziri Mkuu kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa imetoa zawadi mbalimbali kwa kata tatu bora zilizofanya vizuri, shule 10 bora, walimu ambao wanafunzi wao wamepata daraja A katika masomo mbalimbali wanayofundisha pamoja na wanafunzi 10 bora.
Miongoni mwa zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu, kompyuta kwa ajili ya matumizi ya shule zilizofanya vizuri, ikiwa ni kichocheo cha kuongeza bidii ili mwakani wapate matokeo mazuri zaidi.
Awali, akizungumza katika hadhara hiyo, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa aliupongeza uongozi wa mkoa wa Lindi kwa mikakati waliyoiweka kwa ajili ya kuboresha elimu, ambayo imesababisha kupatikana kwa matokeo hayo mazuri.
“Nawapongeza kwa sasa mimi kitaaluma ni mwalimu hivyo nafahamu ili mwanafunzi apate matokeo mazuri ni lazima mwalimu afanye juhudi kubwa zitakazomuwezesha mwanafunzi kufaulu masomo yake.”
Alisema matokeo mazuri ya wanafunzi ndiyo yatakayowafanya walimu wafurahi. “Matokeo haya yasiishie hapa mwakani tuongeze bidii tuweze kupata matokeo mazuri zaidi yatakayotuwezesha kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.”
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa wilaya ya Ruangwa, Mwalimu Selemani Mrope alisema kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 hali ya ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba haikuwa nzuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya utoro.
Mwalimu Mrope alitaja sababu nyingine kuwa ni walimu kutowajibika ipasavyo, ufuatiliaji na usimamizi duni wa taaluma shuleni, ambapo viongozi wengi wa shule na kata walishindwa kusimamia ipasavyo majukumu yao na kuwaacha walimu wafanye kazi kwa mazoea.
“Wazazi wengi kukosa kuwajibika ipasavyo katika elimu ya watoto wao na kuona elimu haina maana kwao na kushindwa kuwahimiza watoto kwenda shule na kusababisha utoro huku wengine wakidiriki kuwashawishi watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani yao.”
Baada ya tathmini waliamua kuweka lengo la ufaulu wa asilimia 80 kwa mwaka huu na asilimia 90 mwaka 2019, hivyo walishirikisha wadau wote wakiwemo viongozi wa Serikali, walimu, wanafunzi, wazazi, viongozi wa dini, wazee maarufu na viogozi wa siasa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, NOVEMBA 18, 2018.