Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Aagiza Taec, Tbs na Tfda Ziharakishe Kutoa Majibu Kwa Wadau Wake
Apr 29, 2019
Na Msemaji Mkuu

*Azindua maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki

*Aagiza watumishi watatu wapandoshwe vyeo kwa kukataa rushwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi zinazofanya uhakiki na upimaji bidhaa nchini zijirekebishe na ziongeze kasi ya utoaji matokeo kwa wateja.

 "Kumekuwa na malalamiko kutoka mipakani juu ya bidhaa zinazochukuliwa ili zikapimwe kwamba zinachukua muda mrefu. Tume ya mionzi, TBS na TFDA ni mioyo mwa taasisi zinazolalamikiwa. Tumieni fursa hii kujirekebisha na kuharakisha utoaji wa matokeo," amesema.

 Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili 29, 2019) wakati akizindua maabara ya Maabara ya kisasa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission -TAEC) iliyopo Njiro, jijini Arusha.

 “Nafahamu kuwa hii Tume inafanya kazi kwa karibu na bandari vituo vya mipakani ili kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Naamini kuanzia sasa mtaharakisha upimaji wa bidhaa na vifaa na kutoa majibu ya vipimo haraka,” amesema.

 Waziri Mkuu ameitaka Bodi na Menejimenti ya Tume, waendelee kubuni na kuibua miradi mingine zaidi ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia. “Angalieni uwezekano wa kuanzisha kinu cha utafiti kinachotumia teknolojia ya nyuklia (Research Reactor); mtambo wa kuongeza thamani na ubora wa vitu mbalimbali ikiwemo matunda na mazao mbalimbali (multi-purpose irradiator); na mtambo wa kuzalisha dawa za kuchunguza na kutibu maradhi ya saratani (accelerator).”

 Amesema kwa kufanya hivyo, maabara hiyo na watumishi wake wataongeza mchango wa teknolojia ya nyuklia kwenye ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

 Amesema anatambua kwamba Tume ya Nyuklia Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa wafanyakazi na ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa maabara awamu ya pili. “Serikali inazichukua changamoto hizo na itaendelea na juhudi za kuzitafutia ufumbuzi kadiri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu,” amesema.

 Waziri Mkuu ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa msaada wa vifaa vya maabara hiyo vyenye thamani ya Euro milioni 2.2 (sawa na sh. bilioni 7.5) na kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika sekta mbalimbali.

 Wakati huohuo, Waziri mkuu ameiagiza Bodi na uongozi wa Tume hiyo wawapandishe vyeo watumishi watatu wa tume hiyo ambao aliwapa vyeti na zawadi ya sh. milioni kwa kukataa rushwa na vitisho.

 “Nimefurahi sana kuona watumishi watatu ambao ni wazalendo na wamekataa kupokea rushwa au kukubali vitisho walivyokuwa wakipewa na kuamua kusimamia misingi ya kazi zao.”

 “Watumishi hawa ni mfano wa kuigwa na wengine. Mwenyekiti wa Bodi waongeze fedha nyingine kila mmoja sh. milioni mbili ili jumla iwe milioni tatu na wapandishwe vyeo huko waliko ili iwe motisha zaidi kwao. Sijui muundo wenu ukoje, lakini nataka nipate taarifa ya utekelezaji wa haya maamuzi kesho kutwa, baada ya Mei mosi,” amesisitiza.

 Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu awape vyeti na zawadi, Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Najjat Mohammed aliwataja watumishi hao kuwa ni Machibya Matulanya wa kituo cha Mtwara na mpaka wa Kilambo (Tanzania) na Msumbiji; Patrick Simpokolwe na Geofrey Kalolo wa kituo cha Tunduma (Tanzania) na Zambia.

 Machibya Matulanya ambaye cheo chake ni mtafiti wa mionzi daraja la pili (Radiation Health Physics Research Officer II) amekuwa akitegewa mitego ya rushwa na kupokea vitisho kutoka wa wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.

 Patrick Simpokolwe ambaye cheo chake ni mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili (Radiation Safety Inspector II) na Geofrey Kalolo ambaye ni mtumishi wa kujitolea (volunteer) naye pia anafanya kazi kama mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili. Wote kwa pamoja walipokea vitisho walipozuia mzigo kutoka Zambia wenye thamani ya zaidi ya milioni 20 usiingizwe nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi