Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Aagiza Dosari za Miradi Rombo Zishughulikiwe
Feb 19, 2026
Waziri Mkuu Aagiza Dosari za Miradi Rombo Zishughulikiwe
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Wakati wa Uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Shule ya Mwalimu Francis Moshi Technical, iliyopo Wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Na Scholastica Sambi – MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amemuagiza Waziri wa TAMISEMI kufuatilia kwa karibu maeneo yenye dosari katika ujenzi wa miradi ya Serikali na kuhakikisha hatua zinachukuliwa mara moja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Februari 19, 2026, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Shule ya Mwalimu Francis Moshi Technical iliyopo wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nchemba amesema miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwamba Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta mbalimbali za maendeleo, hivyo ni wajibu wa wasimamizi kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

“Miradi hii ni kielelezo cha kiongozi mwenye maono. Haya si maono ya kwenye maandishi pekee, bali ni utekelezaji wa vitendo. Ndani ya miaka minne, shule zaidi ya 103 zimejengwa nchi nzima,” amesema Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, wigo wa vyuo vya kati na vyuo vikuu umeongezwa katika mikoa yote, huku kila mkoa ukiwa na shule maalumu ya wasichana. Sambamba na hilo, zaidi ya shule 1,300 za sekondari zimejengwa nchini kote.
Dkt. Nchemba amesisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni uwekezaji unaogusa maisha ya kila familia, kwani unatoa fursa na dira kwa vijana. Amewataka viongozi wa TAMISEMI kuhakikisha hakuna ucheleweshaji katika ukamilishaji wa miradi hiyo ili wananchi wapate huduma kwa wakati.

“Tusiruhusu dosari ndogondogo ziwakwaze wananchi. Miradi ikamilike kwa wakati na itoe matokeo yaliyokusudiwa,” amesisitiza.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi