Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mhagama; Bilioni 16 Zimetumika Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Kigoma na Dodoma.
Dec 19, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na. OWM, Kigoma.

Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Baraza la Taifa la Biashara, kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji unaotekelezwa katika mkoa wa Kigoma na Dodoma, umefanikiwa kuboresha Mazingira ya Biashara na uwekezaji katika mikoa hiyo kwa kutumia  kiasi cha Shilingi bilioni 16 hadi kufikia Desemba 2018.

Mradi huo ambao utekelezaji wake unajikita katika Uwekezaji na Biashara katika Halmashauri kupitia mfuko wa (SIFF), Kuimarisha minyororo ya thamani pamoja na kuimarisha majadiliano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, tayari umefanikiwa kuboresha Mazingira ya Biashara kwa Wakulima na wavuvi wa mkoani Kigoma.

Akiongea katika ziara yake mkoani Kigoma wakati wa kukagua shughuli za utekelezaji za Baraza la Taifa la Biashara, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amefafanua kuwa Baraza la Taifa la Biashara kwa kushirikiana na Mradi huo wameweza Kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia uwekezaji kwenye miradi midogo midogo inayochochea ongezeko la ajira na kipato.

“Nimetembelea Mwalo na Soko la Samaki la Kibirizi, hapa mkoani Kigoma nimeridhishwa jinsi Mradi huu ulivyoboresha miundo mbinu ya mwalo huu katika kuhakikisha wavuvi wanapunguza upotevu wa mazao ya samaki na dagaa. Niyaombe Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya yaendelee na mfumo wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha walengwa wa mradi huu wanaendelea kunufaika” Alisisitiza Mhagama.

Mhagama alifafanua kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kupunguza vikwazo na kero kwa wafanyabiashara lakini pia Kuimarishwa kwa mahusiano kati ya Serikalii na Sekta Binafsi na kuongezeka kwa  ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika Mipango ya Serikali.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Mratibu wa Mradi (Masuala ya Majadiliano ya Sekta ya Umma na Binafsi), Andrew Mhina alibainisha kuwa Mradi huo unalenga kuhakikisha kuwa unaboresha mazingira ya Biashara na  uwekezaji nchini tayari umeandaa mwongozo wa Majadiliano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kuyajengea uwezo Mabaraza ya Mikoa yaweze kuwa endelevu na yenye ufanisi ambapo Baraza la Taifa la Biashara kwa kushirikiana.

Katika ziara hiyo, Waziri Mhagama, pamoja na kutembelea mwalo wa soko la Samaki la Kibirizi waziri alitembelea Kituo cha Biashara (One Stop Business Centre – Kigoma), Soko la Jioni la Mwanga, na Mradi wa Kuwezesha Vijana Kushiriki katika Kilimo Biashara na Mnada wa Mifugo Buhigwe.

   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi