Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema lugha ya Kiswahili inaendelea kuimarika kimataifa na kuwa mhimili wa utambulisho wa Afrika pamoja na chombo muhimu cha kukuza diplomasia, elimu na maendeleo.


Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo alipohutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha-Mama tarehe 20 februari, 2026 yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jijini Paris, Ufaransa ambapo aliwakilisha Serikali ya Tanzania.


Alisisitiza kuwa, zaidi ya watu milioni 500 duniani wanazungumza Kiswahili, jambo linalothibitisha nafasi yake kama lugha ya kimkakati katika diplomasia na uchumi wa kimataifa.



Aidha, aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa UNESCO kwa mchango wake katika kukuza Kiswahili duniani, huku akisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuwekeza katika elimu, tafiti na ushirikiano wa kimataifa ili kuimarisha zaidi hadhi ya lugha hiyo.