Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amenadi fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini katika mkutano wa wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia.
Katika mkutano huo, Waziri Makamba amewaeleza wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini pamoja na mageuzi makubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yanayofanyika chini ya uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Makamba amesema mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na rafiki kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuhakikisha wafanyabiashara wanatekeleza majukumu yao katika mazingira rafiki na salama.
Kadhalika Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania inazingatia misingi ya utawala bora pamoja na kuzungukwa na nchi saba ambazo hazina bandari na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.
Waziri Makamba ameongeza kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ya Tanzania ni salama kwa sababu Tanzania imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni pamoja na Serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi.
“Napenda kuwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Tanzania kwani licha ya kuwa na mzingira salama, pia kuna fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali kama nishati, utalii, kilimo, afya na elimu,” alisema Waziri Makamba.
Kadhalika, Waziri Makamba ameongeza kuwa kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Soko Huru la pamoja la Afrika (AfCFTA) ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.5 hali ambayo itawezesha wafanyabiashara wa Italia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.
Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Italia katika kutekeleza Mpango wa Mattei kwa maslahi ya pande zote mbili, na kuwasisitiza kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na visiwani Zanzibar.
Akiongea awali katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari amesema kuwa utekelezaji wa mpango wa Mattei utakapoanza utazingatia maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau ambapo miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika ikiwemo Tanzania.
Tanzania ni moja kati ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.