Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Katambi Awaomba Viongozi wa Dini Shinyanga Kumuombea Rais Samia
Apr 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Patrobas Katambi amewaomba Viongozi wa dini wa Jimbo la Shinyanga mjini kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani ili aendelee kuitumikia nchi katika kuleta maendeleo endelevu.

Mhe. Katambi ameyasema hayo jana jioni tarehe 24 Aprili, 2022, Mjini Shinyanga, wakati akishiriki futari aliyoiandaa kwa viongozi wa dini ya Kiislamu wa jimbo la Shinyanga mjini. Aliongeza kuwa Mhe. Rais Samia analo jukumu kubwa la kuwaletea Watanzania Maendeleo ili wawe na ustawi bora wa maisha.

“Ninawaomba mliombee Taifa letu, mumuombee Mhe. Rais ambaye anafanya kazi kubwa ya kutuletea maendeleo, amechukua nchi hii katika kipindi kigumu,  tumuunge mkono lakini pia na  viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kwa pamoja, naamini tukishirikiana kwa pamoja tutajaliwa afya njema na tutakuwa na Shinyanga yenye maendeleo bora zaidi”

Aidha, amewaomba viongozi hao kuwakosoa na kuwashauri zaidi kuliko kuwasifia, ili masuala yanayotakiwa kuzingatiwa katika maendeleo yatekelezwe kwa utendaji ulio bora na viongozi wa mkoa huo, kwa ajili ya kuwapatia wanashinyanga maendeleo endelevu.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Wizara ya Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel, aliyeshiriki katika Futari hiyo alimpongeza Naibu Waziri Katambi na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo wanashinyanga. Aidha, alifafanua kuwa Mungu ndiyo nafasi ya kila kitu ambapo mataifa yaliyomweka Mungu mbele yameendelea.

“Mataifa yaliyoendelea si kwa sababu ya rasilimali zao bali ni kwa sababu wamemtanguliza Mungu mbele lakini pia wanazo siri za uumbaji, Siri hizo huwasaidia ubongo wao kufunguka na kufikiri nje ya maono ya kawaida, hali ambayo inasaidia sasa tunaona matokeo kwenye matibabu na sayansi na teknolojia”

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Ismail Habib amemshukuru Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Patrobas Katambi kwa kuaandaa Futari na kujumuika na viongozi hao wa dini. Amefafanua kuwa wataendelea kuongoza maombi kwa ajili nchi na kiongozi mkuu Mhe. Rais Samia.

Katika Futari hiyo iliyohitimishwa kwa Dua maalum iliyoongozwa na Sheikh wa Wilaya hiyo, Sheikh, Soud Katagile, ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema, Viongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, pamoja na Viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya dini katika wilaya hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi