Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe amemtaka mkandarasi Makapo Contractors and General Supplies co. Ltd anayejenga barabara ya Masasi-Mpeta KM 16 na Dott Service Limited anayejenga barabara ya Mtwara- Mlivata KM 50 kukamilisha barabara hizo kwa wakati.
Amesema kuanzia sasa Serikali haitakuwa na muda wa kumwongezea mkandarasi atakayebainika amechelewesha ujenzi kinyume cha mkataba.
“Nimeridhika na ubora wa kazi yenu ni nzuri ila ongezeni kasi ili manufaa ya kuwepo kwa barabara ya lami kwa wananchi wa Mtwara yalete matokeo chanya haraka”, amesema Mhandisi Kamwelwe.
Amesema barabara ya Masasi-Mpeta KM 16 na Mtwara- Mlivata KM 50 ni sehemu ya barabara kuu ya uchumi Mkoani Mtwara yenye urefu wa KM 210 inayoanzia Mtwara mjini kupitia Mlivata, Nanyamba,Tandahimba, Newala hadi Masasi.
“barabara hii ikikamilika kwa wakati itaufungua uchumi wa wakazi wa Mtwara kwa kuongeza fursa za ajira, kilimo na biashara”, amesisitiza Mhandisi Kamwelwe .
Naye mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw, Evod Mmanda ameishukuru serikali kwa kasi yake katika ujenzi wa barabara hiyo ambayo ikikamilika itachochea utekelezaji wa sera ya viwanda, utalii, kilimo na uvuvi na hivyo kuzalisha fursa nyingi za ajira kwa wananchi.
“Tumejipanga kuhakikisha tunashirikiana na mkandarasi MAKAPO na DOTT ili kazi zao ziende kwa haraka na kuiwezesha Serikali kuendelea kujenga barabara za lami katika maeneo ya Nanyamba,Tandahimba,Newala na hivyo kuuunganisha kwa lami mkoa wa Mtwara na wilaya zake.
Waziri wa Mhandisi Kamwelwe yuko mkoani Mtwara kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano na kuhimiza kasi ya ujenzi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO, (OKTOBA 9, 2018).