[caption id="attachment_39333" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akimweleza dhamira ya ziara yake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Colonel Magembe (kushoto) pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, alipowasili wilayani humo Desemba 30, mwaka huu, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.[/caption]
Na Veronica Simba – Ukerewe
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote, kuwasilisha mipango-kazi yao kwa viongozi na wawakilishi wa wananchi wa maeneo wanakofanyia kazi ili waweze kuielewa hivyo kusimamia utekelezaji wake.
Alitoa maagizo hayo jana, Desemba 30, 2018 wilayani Ukerewe akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.
Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Colonel Magembe, Waziri Kalemani alifafanua kwamba viongozi na wawakilishi wa wananchi ndiyo wanawajibika kuisemea serikali, hivyo wanapaswa kuifahamu kwa kina miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao, waweze kuwaeleza wananchi.
“Hili ni agizo kwa wakandarasi wote wa miradi hii nchi nzima, wapatieni viongozi wa maeneo mnayofanya kazi mipango-kazi yenu, wajue nini mnatekeleza, kwa namna gani na kwa kipindi gani ili nao wasaidie kuwaelimisha wananchi wao,” alisisitiza Waziri.
[caption id="attachment_39334" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chabilungo wilayani Ukerewe, Desemba 30, 2018 kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.[/caption]Aidha, alitaja umuhimu mwingine wa viongozi kuelewa mipango-kazi ya wakandarasi kuwa itawawezesha kusimamia ipasavyo utekelezaji wake ikiwemo kuhoji pale ambapo watabaini mkandarasi anasuasua.
Akikagua utekelezaji wa miradi husika katika vijiji vya Chabilungo, Namasabo na Muluseni, ambako pia aliwasha umeme rasmi, Waziri Kalemani aliwasisitiza wananchi kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu ili wapate huduma hiyo na kuutumia umeme katika shughuli za kimaendeleo zitakazoboresha maisha yao.
Alisema, baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kulalamika kuwa serikali haiwapelekei umeme lakini ufuatiliaji unapofanyika inabainika kuwa wengi wao wanakuwa hawajalipia gharama husika.
“Ndugu zangu, lipieni ili muunganishiwe umeme, msibaki kulalamika tu,” alisisitiza.
Waziri pia aliwataka viongozi wa wananchi katika maeneo mbalimbali kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wao ili wafahamu utaratibu wote wanaopaswa kuufuata katika suala la kuunganishiwa nishati ya umeme, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi na kulipia gharama husika.
[caption id="attachment_39335" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kulia) akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Shule ya Msingi Chabilungo wilayani Ukerewe, Desemba 30, 2018, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme. Kulia ni Mkuu wa Wilaya, Colonel Magembe na kushoto ni Mwalimu anayefundisha shuleni hapo.[/caption]Awali, akitoa taarifa ya hali ya umeme katika eneo lake, Mkuu wa Wilaya, Colenel Magembe alimweleza Waziri kuwa kati ya vijiji 76 vya Wilaya hiyo, 40 vimekwishaunganishiwa umeme.
Alimwomba Waziri kuwa, wananchi ambao hawajafikiwa na umeme wapelekewe pia ili waende sambamba na wenzao waliokwishaunganishiwa kwa kuutumia umeme katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Waziri aliahidi kutekeleza hilo huku akiwataka wananchi kuwa na subirá kwani mpango wa serikali ni kuwapatia wananchi wote umeme, zoezi linalotekelezwa hatua kwa hatua.
Waziri Kalemani anaendelea na ziara yake ya kazi aliyoianza Desemba 20, mwaka huu kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika mikoa mbalimbali ambapo anatarajia kuhitimisha Januari 2, mwakani.