Veronica Simba – Arusha
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameagiza kufutwa Mkataba wa kazi wa Mkandarasi, kampuni ya M/s Nipo Group Limited, aliyekuwa akitekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza mkoani Arusha, kutokana na utendaji usioridhisha.
Alitoa maagizo hayo Agosti 15, 2020 kwa Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), akiwa katika ziara ya kazi kijijini Lendikinya, Kata ya Sepeko, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.
Dkt Kalemani alilazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa kazi husika katika maeneo kadhaa ya Wilaya hiyo, ambapo alibaini kuwa Mkandarasi husika ametelekeza kazi hiyo kwa muda mrefu, akiacha nguzo zilizosimikwa pasipo kuvuta nyaya wala kuunganisha umeme.
Akizungumza na wananchi wa Lendikinya, Waziri aliwaeleza kuwa Mkandarasi husika alianza kazi hiyo tangu mwaka 2018 na alipaswa akamilishe mwishoni mwa mwezi huu, lakini utekelezaji wake unasuasua ambapo ana miezi zaidi ya mitatu hajaonekana kazini.
Sambamba na kufuta Mkataba, Waziri pia alielekeza Mkandarasi huyo akatwe asilimia 10 ya malipo yake kutokana na kuchelewesha kazi.
Akiendelea kutoa maelekezo, Waziri aliwataka TANESCO na REA kumpatia kazi hiyo Mkandarasi mwingine mwenye uwezo au ifanywe na TANESCO wenyewe na kuhakikisha inakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba, mwaka huu.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hatua zote zifuate utaratibu wa manunuzi, kisheria na kimkataba.
Katika hatua nyingine Waziri aliagiza kukamatwa na Polisi, kuwekwa ndani na kuhojiwa Mwakilishi wa Mkandarasi huyo aliyekuwepo katika ziara ya Waziri ili atoe maelezo kuhusu pesa ambayo Serikali imelipa kwa kazi husika, imetumika vipi.
Alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Edward Balele kutumia Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwakamata Wakurugenzi wa Kampuni husika ambao hawakushiriki katika ziara hiyo, ili wahojiwe walikopeleka pesa ya Serikali.
“Naagiza wasakwe wale Wakurugenzi wenyewe, maana huyu aliyepo ni mfanyakazi tu, wapatikane na wahojiwe ili watusaidie pesa walizolipwa zimekwenda wapi. Hizi ni pesa za Watanzania.”
Awali, akimkaribisha Waziri kuzungumza na wananchi, Mkuu wa Wilaya alimpongeza Dkt Kalemani kwa ufuatiliaji makini wa kazi ambao umemwezesha kubaini udhaifu wa Mkandarasi husika na kuchukua hatua stahiki zinazolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme kama Serikali ilivyodhamiria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga, waliunga mkono maamuzi ya Waziri na kumwahidi kuwa watatekeleza maagizo yote aliyoyatoa.
Kwa mujibu wa taarifa ya TANESCO Mkoa wa Arusha, iliyowasilishwa kwa Waziri, Mkataba wa Mkandarasi husika ni wa miezi 24 ambao ulianza Machi 2018.
Mkandarasi amefikia asilimia 65 ya kazi husika ambapo kwa mujibu wa Mkataba, alipaswa kuwa amefikia asilimia 92 hadi sasa kwa malengo ya kukamilika Agosti 30, mwaka huu.
Mradi unatarajiwa kusambaza umeme katika vijiji 126 kwa Mkoa mzima na kuunganishia umeme wateja wapatao 5,428.