Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kairuki Ataka Taasisi Binafsi Kuweka Wazi Takwimu Zao
Jun 23, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Said Ameir

Serikali imesema ingependa kuona sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuweka wazi takwimu zao ikiwa ni njia mojawapo ya kuchochea dhana ya uwajibikaji na vita dhidi ya rushwa nchini.

Akifungua Mkutano wa siku moja kuhusu Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi na Takwimu Huria kama kichocheo cha uwajibikaji na vita dhidi ya rushwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angellah Kairuki amesema ushirikiano ambao Serikali inataka kuujenga kati yake na wadau wengine katika takwimu huria ni ule utakaokuwa katika misingi ya uwazi na kuaminiana.

Amesema kuwa ni muhimu kwa washirika wa maendeleo, taasisi za kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali kuweka wazi takwimu zao zikiwemo mikataba, hesabu zao ziliyokaguliwa na manunuzi.

“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutekeleza shughuli zake kwa uwazi hivyo inawaomba wadau wengine nao wafuate nyayo za Serikali kwa kufungua takwimu zake kwa dhamira ya kuimarisha uwazi”, Waziri Kairuki alieleza.

Waziri huyo alisema kuwa Serikali haiwezi kufanyakazi pekee (kwa kujitenga) kwa hivyo suala la kujenga ushirikiano na wadau wengine ni la lazima na kusisitiza kuwa ushirikiano huo sharti uwe katika misingi ya uwazi na kuaminiana.

Alibainisha kuwa Tanzania imeamua kujiunga na mpango wa takwimu huria na inauona mpango huo kama fursa nzuri kwake kuimarisha demokrasia na utawala bora kwani chini ya mpango huo, Serikali imebuni na kuchukua hatua maalum za kuhimiza uwazi na uwajibikaji.

Alitaja baadhi ya mafanikio ya mpango huo wa takwimu huria kuwa ni pamoja na kuanzisha Tovuti ya Takwimu Huria na kutayarisha seti za takwimu 163 ambazo tayari zimeshawekwa katika tovuti na wadau wameanza kuzitumia. Alizitaja takwimu hizo kuwa ni za sekta ya elimu, afya na maji.

Waziri Kairuki alitumia fursa hiyo kuwashukuru waandaaji wa mkutano huo pamoja na wafadhili wakiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Maendeleo la Uingereza(DfID) ambao alisema michango yao imeiwezesha Tanzania kuwa kinara katika  Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa uwazi na masuala ya takwimu huria katika bara la Afrika.

Awali akimkaribisha Waziri kufungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu (NBS) Dk. Albina Chuwa aliwashukuru washiriki wa mkutano huo ambao ni miongoni mwa wadau wakuu wa takwimu kwa ushirikiano wao kwa miaka miwili sasa, tangu kufanyika Mkutano wa Kwanza wa Afrika wa Takwimu Huria uliofanyika hapa nchini  ambao ulihudhuriwa na washiriki wengi.

Alibainisha kuwa tangu kufanyika kwa mkutano huo, wadau hao wameshiriki katika kutayarisha Tovuti ya Takwimu Huria ambamo takwimu za sekta za afya, elimu na maji zimeweka wazi kwa matumizi ya kila mtu.

Kazi nyingine walizofanikiwa kuzifanya kwa pamoja ni kutayarisha Rasimu ya Sera ya Takwimu Huria, Mkakati wa Utekelezaji wake na Mkakati wa Mawasiliano. Aidha alieleza kuwa baadhi ya wadau hao walifanikiwa kusaidia katika kujenga uwezo wa baadhi ya taasisi katika kuandaa na kuchapisha takwimu huria.

Dk. Chuwa aliwahakikishia wadau hao kuwa pamoja na ufadhili wa mradi huo kupitia Benki ya Dunia kuwa utamalizika mwezi ujao, Serikali na NBS zitaendelea kufanya kazi na wadau wapya ili kuhakikisha kuwa kazi ya uzalishaji na usambazaji wa takwimu pamoja na kuimarisha ubora wake inafanyika.

Akizungumza kufunga mkutano huo, Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa NBS, Irenius Ruyobya alieleza kuwa Sera ya Takwimu ambayo imo katika hatua za mwisho kukamilika imepitia hatua zote za ushirikishwaji wadau kama taratibu zinaelekeza.

“Mchakato wa utungaji Sera umepitia hatua zote za uwashirikishwaji wadau kwa njia mbalimbali zikiwemo mikutano na kupitia mitandao ambao mwitikio ulikuwa mkubwa”, alisema na kusisitiza kuwa utaratibu ni kuwa rasimu ya Sera haiwezi kufikishwa ngazi za maamuzi bila ya kipengele cha ushirikishwaji wadau kutekelezwa.

Aidha, Bwana Ruyobya aliwaeleza washiriki kuwa Sheria ya Takwimu haipo kuwadhibiti wakusanya takwimu bali jukumu lake kubwa ni kuratibu utoaji wa takwimu rasmi za Serikali au zile ambazo zitatumiwa katika kutolea maamuzi, ufatuatiliaji na utekelezaji wa mipango ya Serikali.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa wanatakwimu wote ni “wadau wa NBS”  na kusisitiza kuwa kumekuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya Ofisi yake na wadau mbali mbali wa takwimu lengo likiwa ni kuhakikisha takwimu wanazozitoa zinakidhi viwango na vigezo vilivyowekwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi