Na Jonas Kamaleki-MAELEZO, Dodoma
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Andrew Massawe kusimamia ipasavyo mifuko mipya ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha michango ya watumishi inakusanywa.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa kikao cha kumpokea Katibu Mkuu huyo aliyeteuliwa hivi karibuni.
“Katibu Mkuu nakuagiza uhakikishe michango inakusanywa na malipo yanalipwa kwa wakati ili kuondoa changamoto kwa wanufaika ikiwemo wastaafu”, alisema Mhagama.
Waziri Mhagama amemtaka Katibu Mkuu kusimamia vizuri uwekezaji uliofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii kabla ya kuunganishwa. Ametaja uwekezaji huo kuwa ni kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Magereza cha Karanga, Moshi, kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari cha Mkulazi.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kiwanda cha sukari kitaongeza ajira hasa kwa vijana na kuongeza fedha za kigeni kwani uagizaji wa sukari toka nje utapungua.
Kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha tani 250 kwa mwaka, ambazo zikiunganishwa na uzalishaji wa viwanda vingine vya sukari nchini zitaondoa uhaba wa bidhaa hiyo.
Amemwagiza pia Afisa Masuhuli wa Wizara hiyo kuangalia kwa makini na kuondoa changamoto za vibali vya kazi na ukaazi kwa wageni. Mhagama amesema eneo hilo lina matatizo makubwa ambayo yanahitaji kushughulikiwa haraka ili kuvutia wawekezaji.
Eneo jingine ambalo Waziri Mhagama amesisitiza lipewe kipaumbele ni uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa ambalo lina lengo la kuwawezesha vijana kutatua changamoto zao ikiwemo ajira.
Zaidi ya asilimia 50 ya nguvu kazi nchini ni vijana hivyo inabidi wapewe kipaumbele, alisisitiza Waziri Mhagama.
“Vijana ni lazima wawezeshwe kushiriki katika uchumi wa nchi yetu kwani ndio idadi kubwa na ndio wenye nguvu”, alisema Mhagama.
Alisisitiza kuwepo na usimamizi madhubuti ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ili kutatua changamoto walizonazo. Waziri Mhagama amempongeza Mhe. Stella Ikupa (Naibu Waziri, Wenye Ulemavu) kwa kusimamia vizuri masuala ya Watu Wenye Ulemavu.
Kwa upande wake, Prof. Andrew Massawe amesema ataanza kushughulikia masuala ya mifuko na kutatatua changamoto zilizopo na zitakazojitokeza.
Amesema kuwa yeye ni mtu wa mifumo, hivyo katika utendaji wake atataka matokeo zaidi kwa kazi za kila siku.
“Madokezo yasiyo na matokeo yasiletwe kwangu, mimi ninachotaka ni kufanya kazi kwa ufanisi na tija ionekane”, alisema Prof. Massawe.
Prof. Massawe ameteuliwa hivi karibuni na kuapishwa tarehe 1, Agosti 2018 na Mhe. John Pombe Magufuli , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.