Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Ateta na Balozi wa Sweden Nchini
Sep 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Bi. Charlotta Ozaki Macias leo Septemba 2022 katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam.  

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo yao yalihusisha ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Sweden katika utekelezaji wa miradi ya utunzaji na hifadhi ya mazingira.

Balozi Charlotta alielezea miradi ya matumizi ya nishati mbadala inayotekelezwa kwa ufadhili wa Sweden kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Aidha, alielezea jinsi nchi hiyo ilivyojizatiti kushirikiana na mataifa ya Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hususan katika kushiriki Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika nchini Misri Novemba, 2022.

Katika kikao hicho, Balozi Charlotta aliambatana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Scania Tanzania, Bi. Johanna Lind ambaye aliwasilisha mpango wao wa kuingiza malori aina ya Scania yanayotumia gesi (Compressed Natural Gas -CNG) na BIOGAS badala ya Diesel kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na uchafuzi wa mazingira.

Alisema matumizi ya gesi ni rahisi na nafuu zaidi kuliko dizeli huku akielezea changamoto iliyopo ni gharama zitokanazo na kodi na vituo vya kujazia gesi ambapo uwekezaji unahitajika.

Waziri Jafo alimshukuru balozi huyo kwa ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Sweden hususan kwa mchango wa nchi hiyo katika sekta mbalimbali za maendeleo ya Tanzania na kuahidi kuendeleza uhusiano huo mzuri hasa katika eneo la Mazingira.

Pia, aliipongeza kampuni hiyo kwa kuja na mpango wa matumizi ya gesi katika magari yao na kuahidi kupata ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mpango huo na ikiwezekana uingizwe katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (DART).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi