Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Nørgaard Dissing-Spandet jijini Dodoma leo Machi 18, 2024.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Jafo amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili na inatarajia kuendelea kushirikiana zaidi katika hifadhi ya mazingira.
Amesema kuwa Tanzania inashirikiana na Denmark katika kusukuma mbele ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo itasaidia katika kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Kupitia ajenda hiyo, amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ameonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha asilimia kubwa ya wanawake wa Tanzania na Afrika kwa ujumla wanatumia nishati safi ya kupikia.
Dkt. Jafo amesema kuwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu, Rais Dkt. Samia alizindua Mradi wa Nishati Safi ya kupikia itakayowasaidia wanawake barani Afrika.
Kutokana na umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, Waziri Dkt. Jafo amesisitiza ni wakati sasa Tanzania inahitaji kuwabadilisha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
Aidha, amewashukuru wawekezaji wa nishati safi ya kupikia hususan gesi kwa kuunga mkono serikali kwa kutoa mitungi ya gesi kwa taasisi mbalimbali zinazolisha watu zaidi ya 100.
Halikadhalika, Dkt. Jafo amesema Tanzania inatekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira ambapo ilizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032).
Kwa upande wake Mhe. Balozi Dissing-Spandet amemuhakikishia Waziri Jafo kuwa nchi yake itaendeleza ushirikiano wake kwa Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ya mazingira.