Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Ataka Kasi ya Usimamizi Biashara ya Kaboni, Nishati Safi ya Kupikia
Apr 05, 2024
Waziri Jafo Ataka Kasi ya Usimamizi Biashara ya Kaboni, Nishati Safi ya Kupikia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisalimiana na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) kwa ajili ya kumkaribisha Mhandisi Luhemeja mara baada ya kuwasili katika ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais zilizopo Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam Aprili 4, 2024 na kujitambulisha kwa viongozi na watendaji kufuatia uhamisho wake kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu). Katikati ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano), Bw. Abdallah Hassan Mitawi
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja kuimarisha kasi ya usimamizi wa biashara ya kaboni, ajenda ya nishati safi ya kupikia na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Sura 191 ili kuhakikisha sekta ya mazingira inaleta tija kwa Watanzania.

Dkt. Jafo amesema hayo Aprili 4, 2024 wakati wa utambulisho wa Katibu Mkuu Mpya wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja aliyehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu).

Mhe. Jafo amesema majukumu ya ofisi hiyo yamezidi kufahamika kwa haraka zaidi na Watanzania kutokana na manufaa yake kugusa maslahi moja kwa moja ya jamii huku akitolea mfano ajenda ya nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa Serikali imepanga kuja na mkakati mahsusi wa kuwakomboa wanawake katika kuachana na nishati chafu ya kupikia.

Akifafanua zaidi Dkt. Jafo ameeleza kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake wa Kitanzania, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo ikiwemo kupunguza gharama ya ununuzi wa vifaa na tayari wadau wengi wameonesha dhamira ya kuunga mkono juhudi hizo.

“Mnakumbuka kuwa Ofisi yetu imepewa maelekezo na Mhe. Rais ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake ifikapo mwaka 203. Hivyo hatuna budi kuandaa mkakati mahsusi wa kuhakikisha kuwa dhamira hiyo inafikiwa na kutekelezeka”, amesema Dkt. Jafo.

Aidha, Dkt. Jafo amesema mwezi Mei mwaka huu kutafanyika mkutano mkubwa utakaojadili ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini Ufaransa na kupitia mkutano huo Serikali ya Tanzania imejipanga kutumia fursa hiyo kuonesha jitihada mahsusi ilizochukua katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake.

Akizungumzia Biashara ya Kaboni, Dkt. Jafo amesema Serikali imeandaa kanuni na mwongozo wa biashara hiyo kupitia usimamizi wa Kituo cha Kitaifa cha Uratibu wa Kaboni (NCMC) kilichopo Mkoani Morogoro ambapo wawekezaji mbalimbali wamejitokeza kwa ajili ya uwekezaji na hivyo mkakati uliopo kuhakikisha jamii inajitokeza na kushiriki katika biashara ili kujiongezea kipato.

Ameongeza kuwa katika kujenga hamasa kwa jamii kushiriki katika biashara ya kaboni, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imepanga kuendesha makongamano na mijadala mbalimbali itakayoshirikisha Viongozi Wakuu wa Serikali pamoja na wadau wa sekta ya mazingira na kuandaa mpango mkakati wa pamoja utakaoinisha fursa na manufaa ya biashara hiyo kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema hadi sasa jumla ya kampuni 42 tayari zimesajili miradi ya biashara ya kaboni katika kituo cha NCMC na kuongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imejipanga kuhakikisha makampuni mengi zaidi yanajitokeza kusajili miradi yao sambamba na kuhimiza ushirikiano wa karibu na wadau wa biashara ya kaboni.

Kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191, Waziri Jafo amesema Serikali imeanza kufanya marekebisho ya kubadili muundo wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia kwa Waziri Jafo) pamoja na Watendaji Waandamizi wa Ofisi hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa shughuli ya utambulisho wa Mhandisi Luhemeja katika Ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais zilizopo Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam Aprili 4, 2024.

Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuwa hadi kufikia Juni 2024, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 itawasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua zaidi.

“Marekebisho hayo yatahusisha kubadili muundo wa NEMC ili kuwa Mamlaka na hatua hiyo itaweizesha kutekeleza majukumu yake kwa nguvu zaidi na hivyo kuleta tija iliyokusudiwa katika suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini” amesema Dkt. Jafo.

Kuhusu masuala ya Muungano, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu na kusimamia vyema utatuzi wa hoja ambapo katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 jumla ya hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kupitia vikao vya kamati ya pamoja baina ya SJMT na SMZ. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amemshukuru Waziri Jafo kwa maelekezo aliyotoa na kuahidi kusimamia utekelezaji wake kwa kushirikiana na watendaji wengine wa ofisi hiyo ili kufikia dhamira na malengo yaliyopo  katika kuwahudumia wananchi.  

Kikao hicho kilihudhuria pia na Watendaji mbalimbali wa Ofisi ya Makamu wa Rais akiwemo Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasimali Watu, Bw. Elisha Msengi, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi