Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Dkt. Mabula Amshukuru Rais Samia kwa Pesa za Programu ya Upimaji Ardhi
Sep 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, MWANZA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt Angeline Mabula amemshukuru Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa  kuiwezesha wizara yake kupata fedha kiasi cha Shilingi bilioni 50 kwa ajili ya programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliipatia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuzikopesha Halmashauri 55 kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi nchini. 

Alisema, utolewaji wa kiasi hicho cha fedha kumewezesha Mkoa wa Mwanza kupatiwa Shilingi Bilioni 6.691 zilizosaidia kutekeleza miradi ya kupanga, kupima na  kumilikisha ardhi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. 

Dkt. Mabula ametoa shukran hizo tarehe 13 Septemba, 2022 jijini Mwanza mbele ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Phillip Isdori Mpango wakati wa uzinduzi wa stendi mpya na ya kisasa ya mabasi na maegesho ya malori iliyopo eneo la  Nyamhongolo wilayani  Ilemela.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, uwezeshwaji wa pesa uliofanywa na Serikali katika sekta ya ardhi umeisadia Halmashauri yake ya Manispaa ya Ilemela kuwa na mradi wa kuuza viwanja alioueleza kuwa umeonesha mafanikio makubwa.

 "Kuhusu masuala ya ardhi, ninamshukuru Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wizara Shilingi bilioni 50 na kati ya kiasi hicho mkoa wetu wa Mwanza umepata bilioni 6.91 pesa ambazo zimeisadia sana zoezi la upimaji viwanja katika halmashauri zetu ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela" alisema Dkt. Mabula.

Hata hivyo, Dkt. Mabula ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza alisema, mbali na Mhe Rais Samia kuisadia  sekta ya ardhi  lakini kuna juhudi kubwa zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Mwanza hususan kwenye masuala ya miundombinu, uchukuzi pamoja na huduma za afya jambo alilolielezea kuwa, limejenga imani kwa wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi