Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amekutana na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Luteni Jenerali Mathew Mkingule na kufanya mazungumzo juu ya kuboresha ushirikiano baina ya wizara yake na Jeshi kwenye masuala mbalimbali ya michezo ikiwemo wataalamu, miundombinu ya michezo na usafiri.
Katika kikao hicho kilichofanyika Agosti 31, 2021 jijini Dodoma, Waziri Bashungwa amemweleza Mnadhimu huyo nia ya Wizara ya Habari kushirikiana na jeshi hilo katika kuinua sekta ya michezo kwa kuwashirikisha wataalamu mbalimbali wa michezo ambao wapo katika majeshi mbalimbali hapa nchini ili waweze kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo.
Waziri Bashungwa amesema Wizara yake imeona ni vyema kuwa na michezo ya kikamkati (Kipaumbele) ili kujikita zaidi kwenye michezo hiyo na kuweza kushindana kimataifa, akisema kufanya hivyo kutairudisha Tanzania katika historia ya baadhi ya watanzania waliowahi kufanya vyema katika baadhi ya michezo kimatafifa.
“Tunaamini kwa kushirikiana na jeshi, timu za Taifa zitaweza kufanya kambi katika maeneo ya jeshi, hii itaongeza nidhamu na ukakamavu wa timu zetu” Amesem Waziri Bashungwa.
Kwa upande wake Luteni Jenerali, Mathew Mkingule amesema mazungumzo hayo ni hatua nzuri katika kukuza sekta ya michezo akisema anaipeleka taarifa ya mazungumzo hayo kwa Mkuu wa Majeshi kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Aidha, viongozi hao kwa pamoja wamekubaliana kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kukutana na uongozi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) ili kujadiliana namna bora na sehemu za kipaumbele za kushirikiana.