Na: Mwandishi Wetu -MAELEZO
Serikali imesema haiwalazimishi wakimbizi raia wa Burundi kurejea nyumbani bali ni maamuzi yao wenyewe baada ya wao wenyewe kujiridhisha kuwa hali nchini mwao ni shwari, tulivu na salama.
Akizugumza mwishoni wa Mkutano wa 19 wa Kamisheni ya pande tatu kuhusu wakimbizi wa Burundi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba aliuambia mkutano huo kuwa wakimbizi wote waliojiandisha kurejea nyumbani walifanya hivyo kwa ridhaa yao wenyewe pasi na shindikizo kutoka Serikali si ya Tanzania wala ya Burundi.
“Hakuna shinikizo lolote… wanafanya tathmini wao wenyewe kwa kuwasiliana na ndugu na jamaa zao walioko Burundi na wako wengi ambao wamerejea nyumbani kwa hiari yao na kwa njia zao wenyewe bila hata ya kufuata utaratibu huu tunaouandaa sisi” alieleza Waziri Mwingulu.
Alibainisha kuwa Tanzania ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika (AU) imeridhia mikataba mbali mbali ya kimataifa kuhusu wakimbizi hivyo haiwezi kufanya hivyo na kusisitiza kuwa Tanzania daima imekuwa mwanachama wa mfano katika kutekeleza mikataba hiyo.
Waziri Mwigulu aliongeza kuwa kutokana na baadhi ya wakimbizi kuona wanacheleweshwa kurejeshwa nyumbani wakati mwingine hujikusanya na kusababisha hata vurugu makambini ili hatua za kuwarejesha ziharakishwe ili waweze kuondoka na kuwahi msimu wa kilimo nchini kwao.
Waziri huyo wa Mambo ya Ndani aliwaeleza waandishi wa habari pembeni mwa mkutano huo kuwa wanatarajia wakimbizi wengi zaidi kujiandikisha baada ya zoezi la kuwarejesha nyumbani litakapoanza.
“Kuchelewa kuwarejesha wakimbizi waliojiandikisha kumewafanya wakimbizi wengine kusita kujiandikisha lakini wakati makundi ya kwanza yatakapoanza kuondoka hiyo itakuwa motisha kwa wengine zaidi kujiandikisha”Alifafanua Waziri Mwingulu.
Wakati huo huo, Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) wamepitisha mpangokazi wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi raia wa Burundi ambao tayari wamejiandikisha kwa hiari kurejea nyumbani.
Mpangokazi huo ni sehemu ya makubaliano yaliyotiwa saini jana kufuatia Kikao cha 19 cha Kamisheni ya Pande Tatu kilichofanyika jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na mawaziri wanaoshughulikia wakimbizi wa Tanzania, Burundi na mwakilishi wa UNHCR.
Chini ya Mpangokazi huo wa kipindi cha karibu miezi mine (07 Septemba hadi 31 Disemba, 2017) wakimbizi 12,000 ambao tayari wamejiandikisha kwa hiari watarejeshwa nyumbani huku ukitoa nafasi kwa wengine zaidi watakaojiandikisha kujumishwa.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo wa Burundi Pascal Barandagiye na Mwakilishi wa UNHCR nchini Bibi Chansa Ruth Kapaya.
Chini ya Makubaliano hayo shirika la UNHCR na washirika wake wataweza kutembelea maeneo ya mipakani ya Tanzania na Burundi kwa lengo la kusaidia mchakato wa urejeshaji wa hiari wa wakimbizi hao na masuala mengine yanayohusu hifadhi ya wakimbizi na raia wengine wanaohitaji hifadhi.
Pande hizo za makubaliano zimetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano katika kutekeleza zoezi la kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao na kulitaka shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kutoa chakula kwa wakimbizi wanaorejea kwa kipindi cha miezi mitatu.
Kikao hicho cha 19 cha Kamisheni ya Pande Tatu kimeeleza kutumbua na kuthamini ukarimu wa watanzania ambao umewezesha mamilioni ya wakimbizi kuishi Tanzania tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1961 na zaidi kuendelea kuwakarimu wakimbizi wapatao 350,000 miongoni mwao 256,850 wakiwa raia wa Burundi.