Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dar es salaam na Pwani kwa kutembelea matanki makubwa ya uhifadhi maji, mtambo wa uzalishaji maji wa Ruvu Chini ili kujionea hali ya uzalishaji maji na usambazaji ilivyo Ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za wizara hiyo kupunguza changamoto ya upungufu wa maji uliojitokeza kutokana na kuchelewa kwa mvua.

Waziri Aweso amewasihi wananchi kujenga utamaduni wa kuwa na vyombo vya kutunza na kuhifadhi maji katika kipindi hiki na ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kushirikiana na wadau binafsi wenye visima vikubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma.

Pia Waziri Aweso ameongeza kwa kutoa maagizo kwa DAWASA kuhakikisha visima vyote vilivyochimbwa na Serikali vinaingizwa kwenye mfumo wa usambazaji ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa Wananchi